RAIS SAMIA APONGEZWA KWA USHIRIKIANO NA TAASISI ZA DINI
#KAZIINAONGEA
Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge -Ngara, Mhashamu Severine Niwemugizi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwasaidia kufanya harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Rulenge -Ngara mkoani Kagera na kuwa hatua hiyo inadhihirisha upendo wa dhati wa Rais kwa wananchi wa Ngara na Watanzania kwa ujumla.
Askofu ameyasema hayo Februari 22, 2025 jijini Dar es Salaam wakati alipofanya harambee ya ujenzi wa Kanisa hilo. Awali akizungumza wakati wa misa takatifu Askofu amehabarisha,
“ Katika kujenga nyumba ya bwana tulipopiga hodi kwa Mhe. Rais Samia kumuomba atusaidie kujenga nyumba ya heshima ya bwana alikubali na tunafurahi jioni hii amemtuma Dkt. Biteko awe nasi, tumtukuze Mungu katika ushirikiano huu anaouweka na kwamba viongozi wa Serikali wako tayari kusaidia watu katika kutimiza nia zao,” amesema Askofu Niwemugizi.
Aidha Askofu amesema kuwa, Jimbo hilo liliundwa mwaka 1960 na kwa sasa linajumuisha Wilaya za Biharamulo, Chato na Ngara.
Pia ameongeza kuwa, Kanisa lililopo lilianza kama kigango na limekuwa likipanuliwa mara kwa mara kulingana na mahitaji.
Ameendelea kwa kusema, wamefikia uamuzi wa kujenga kanisa jipya ili kukidhi mahitaji ya sasa.
Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amempongeza Askofu Niwemugizi kwa maono ya kujenga Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Rulenge - Ngara mkoani Kagera.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo alipohudhuria harambee hiyo na kusema,
“ Nakupongeza baba Askofu kwa kuwa na maono makubwa ya kujenga hekalu la bwana la viwango vya juu na kuwaza makubwa,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea “ Binafsi namuona Baba Askofu kama mbeba maono wa Jimbo na sisi tumshike mkoni ili nia yake iweze kufanikiwa. Kiu hiyo itafanikiwa kwa kuwa nia ipo na kanisa litajengwa na sisi wenyewe,”
Aidha, Dkt. Biteko amemshukuru Rais Samia kwa kumpa fursa ya kumwakilisha kushiriki katika tukio hilo la harambee ya ujenzi wa kanisa.
Kwa upande wake Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa Kanisa hilo, Daudi Masaka amesema kuwa ujenzi wa kanisa hilo hadi kukamilika kwake utagharimu jumla ya shilingi bilioni 7,700,000/=
Aidha, ametaja baadhi ya sehemu ya kanisa hilo kuwa sakafu ya pili ya jengo litakuwa na uwezo wa kubeba watu 2100, makanisa madogo mawili na sehemu ya makaburi manne.
Aidha, harambee hiyo imehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments