MOROGORO WAZINDUA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI KWA WAFUGAJI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limezindua Kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili katika viwanja vya shule ya Msingi Wimidakawa vilivyopo Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro eneo ambalo wakazi wake wengi ni wafugaji
Uzinduzi huo umefanyika Novemba 30, 2024 Mgeni rasmi akiwa ni Kamishina Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) Linus Mnyambwa aliyemuwakilisha Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro ambapo amesema, Kampeni hii ni ya kila mwaka inayoanza Novemba 25 hadi Disemba 10 yenye lengo la kupinga ukatili na kutetea haki za wanawake.
Kamishina Mnyambwa amesema, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeona ipo haja ya kuongea na jamii ya wafugaji ambayo imekuwa ikiathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukatili na ndio sababu ya kuzindua katika eneo la Dakawa lenye wakazi wengi jamii ya wafugaji.
Aidha, amesema kwa upande wa Jeshi la Polisi lishajipanga sawasawa kukabiliana na vitendo hivyo kilichobaki ni wananchi kutoa taarifa kwa wingi ili zifanyiwe kazi na kupunguza matukio hayo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Morogoro Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Dkt Mwanaid Lwena amesema, Ukatili unaowatesa wafugaji ni wa kurithishwa wanaume bila ridhaa endapo mke atafiwa na mume jambo ambalo linapigwa vikali na haliruhusiwi kisheria.
Anna Almasi (49) Mwenyekiti wa Wamama Wafugaji amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwapa kipaombele katika uzinduzi huu kwani jambo hilo litawapa ujasiri wa kutoa taarifa za ukatili zinazowatesa kwa muda mrefu.
Wadau wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Dakawa na wenyeviti wa vitongoji, Taasisi ya msaada wa kisheria, Viongozi wa dini na wananchi huku kauli mbiu ya mwaka huu ikisema "Miaka +30 ya Beijing chagua kutokomeza uhalifu"
Mwisho
0 Comments