MRADI WA MAEGESHO CHIMBUYA KULETA UNAFUU KWA WANANCHI, WASAFIRISHAJI
#KAZIINAONGEA
Mradi wa ujenzi wa maegesho ya Chimbuya Wilayani Tunduma Mkoani Songwe, unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, unatarajiwa kuwa mkombozi kwa wafanyabiashara katika kutatua msongamano wa magari katika barabara ya TANZAM.
Mradi huo ambao ni miongoni mwa miradi iliyofanikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Samia, unahusisha ujenzi wa eneo la Maegesho lenye urefu wa mita 50 na upana wa mita 46, ufungaji wa taa za barabarani kwa urefu wa zaidi ya kilometa tatu, pamoja na ujenzi wa vyoo, bafu, uzio, na ofisi.
Mradi huu ambao utaleta matumaini mapya kwa wasafiri na wafanyabiashara umegharimu Shilingi Bilioni 1.8 na ukarabati wake umefikia asilimia 90 ya utekelezaji wake.
Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alitoa mwezi mmoja kwa TANROADS Mkoani Songwe kukamilisha ujenzi wa kituo cha maegesho katika eneo la Chimbuya ili kufikia wiki ya kwanza ya mwezi wa Disemba, maegesho hayo yaanze kutumika kwa kupunguza foleni ya malori kukaa barabarani.
Katika maelekezo hayo pia amemuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kufunga mizani mitatu inayohamishika (Mobile Weighbridge) ya kudhibiti uzito wa magari katika eneo la Tunduma ili kuongeza kasi ya upimaji wa magari na kupunguza msongamano wa malori yanayosubiria kwa muda mrefu kupima katika mzani mmoja wa Mpemba unaopima Magari yanayoelekea Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Kukamilika kwa kituo hicho cha maegesho, kutatoa urahisi kwa Wasafarishaji na wananchi katika eneo hilo kutokana na msongamano wa malori wa muda mrefu na kukwamisha matumizi ya barabara kwa watumiaji wengine.
#KAZIINAONGEA
0 Comments