POLISI YAWASHIKILIA WAWILI MAUAJI YA MWENYEKITI UVCCM CHUNYA.

 

POLISI YAWASHIKILIA WAWILI MAUAJI YA MWENYEKITI UVCCM CHUNYA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Tawi la Machinjioni Kata ya Bwawani Michael Andarson Kalinga [36] mkazi wa Makongolosi Wilayani Chunya kwa kumpiga na kitu butu kichwani.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Wilbert Siwa amesema tukio hilo limetokea  Desemba 02, 2024 saa 5:30 usiku huko Mianzini, eneo la Mikoroshini, Wilaya ya Chunya.

Amesema marehemu   Kalinga [36] alikutwa amefariki dunia na mwili wake kutelekezwa porini umbali wa mita 250 kutoka barabara ya Makongolosi kuelekea Lupatingatinga.

Amesema marehemu alifariki dunia  baada ya kupigwa na kitu butu kichwani sehemu ya utosini na  kufanikiwa kumpora Pikipiki yenye namba za usajili MC.464 ELL aina ya Kinglion.

Amesema Jeshi la  Polisi lilifanya msako mkali ambapo Desemba 03, 2024 huko Mlowo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao wanatuhumiwa kuhusika na tukio hilo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa onyo kwa baadhi ya wananchi ambao wanaendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi na badala yake wafanye kazi za kihalali

Post a Comment

0 Comments