RAIS DKT. SAMIA AELEKEZA FEDHA ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 63 YA UHURU ZIKATOE HUDUMA ZA JAMII

RAIS DKT. SAMIA AELEKEZA FEDHA ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 63 YA UHURU ZIKATOE HUDUMA ZA JAMII

#KAZIINAONGEA

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza fedha zote za maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Mwaka 2024 zielekezwe kwenye huduma za jamii.

Aidha ametaka maandalizi ya maadhimisho hayo yafanyike katika ngazi ya mikoa na Fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwa ajili ya Maadhimisho hayo zielekezwe katika kutoa huduma.

Rais Dkt. Samia ameelekeza kuwa kila mkoa uhakikishe Wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii kama vile kwenye Masoko, Hospitali, Kambi za wazee na wenye mahitaji maalum, mashindano ya michezo mbalimbali pamoja na makongamano na midahalo ya kujadili maendeleo endelevu yaliyopatikana kwa miaka 63 ya Uhuru.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Disemba 04, 2024, katika kikao kazi cha Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. 

“Sherehe za mwaka huu hazitakuwa na Gwaride na Shughuli nyingine za Kitaifa”.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inatoa wito kwa Wananchi kushiriki katika shughuli hizo ili kujivunia sifa za kipekee ambazo zimetokana na Uhuru wetu. 

“Ninatoa rai kwa Wakuu wote wa Mikoa ya Tanzania Bara, kuzingatia na kufuata ipasavyo maelekezo Mahsusi yaliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha Maadhimisho haya yanafanyika kwa ufanisi kwa lengo la kuuenzi Uhuru wetu.”

Ameongeza kuwa shughuli za Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ya Mwaka 2024 zilishaanza tangu Disemba 2, 2024 na zitafanyika mpaka Disemba 9,2024 ambayo ni siku ya kilele cha Uhuru wa Tanganyika uliopatikana Disemba 9,1961.

“Katika Maadhimisho haya, Taasisi zote za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama zinaelekezwa kuhakikisha Majengo yote ya Serikali Tanzania Bara yanapambwa kwa vitambaa vya rangi ya Bendera ya Taifa, picha rasmi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni muasisi wa Uhuru wetu pamoja na picha ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo ya mwaka huu ni: Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara: “Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa maendeleo yetu”

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments