USIMAMIZI MZURI WA FEDHA UTAJENGA TABIA KWA WANANCHI KULIPA KODI KWA HIARI
#KAZIINAONGEA
Katika kuhakikisha Watanzania wanakuwa na mwitikio mzuri na uhiari katika suala zima la ulipaji kodi mbalimbali hapa nchini kwa maendeleo ya Taifa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Fedha imewataka watu wa fedha, kujenga imani kwa Umma katika Mifumo ya Usimamizi wa fedha ili kujenga tabia kwa wananchi kulipa kodi kwa hiari.
Akizungumza katika Mkutano wa Pili wa Mwaka wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Nchi za Afrika (AAAG) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Desemba 2, 2024 Jijini Arusha, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, usimamizi mzuri wa fedha unajenga tabia ya wananchi kulipa kodi kwa hiari.
“Kwetu sisi watu wa Wizara ya Fedha, nchi zote za Afrika, jukumu letu hasa ni la kujenga imani kwa Umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha ili kujenga imani kwa wananchi ndio msingi unaowezesha walipa kodi kulipa kwa hiari.” amesema Waziri Nchemba.
Dkt. Nchemba ameongeza kuwa, bila usimamizi mzuri wa fedha, hakuna rasilimali zinazoweza kupatikana, kuboreshwa au kuwekezwa kwa ufanisi na kwamba watu wanapokuwa na imani na usimamizi wa fedha, wanajenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari kwa sababu wanajua fedha zao zinakwenda wapi.
#KAZIINAONGEA
0 Comments