WANANCHI RUKWA KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewasogezea huduma za Kibingwa Wananchi wa Mkoa wa Rukwa, kwa kuweka kambi ya Madaktari Bingwa 33 kutoka Kanda ya Magharibi, watakaotoa huduma kwa wakazi wa Mkoa huo na nchi jirani, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga.
Kuwepo kwa kambi ya Madaktari hao, ni jitihada zinazofanywa na Rais Samia katika kipindi cha miaka mitatu, tangu alipoingia madarakani katika kuboresha huduma mbalimbali kwa Watanzania ikiwemo huduma ya afya.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala wa Mkoa, Msalika Makungu amesema kuwa, huduma hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi na kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa ambao kawaida wanahitaji rufaa kwenda maeneo mengine ili kupata huduma za kibingwa.
Ameongeza kuwa, wananchi wa Mkoa wa Rukwa wana uhitaji mkubwa wa huduma za Kibingwa hivyo, amewataka madaktari hao kutoa huduma hizo kwa ufanisi ili kuhakikisha wanapata matibabu bora kwa wakati.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Ibrahim Isack, amesema kuwa huduma hii ni fursa nzuri kwa madaktari wa Mkoa kujifunza na kuboresha ufanisi wao katika utoaji wa huduma za kibingwa kupitia wataalamu hao wanaotoa huduma katika kambi hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga, Dkt. Ismail Macha, amesema kuwa lengo la zoezi la huduma mkoba ni kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi na kupunguza rufaa za magonjwa ambayo hayana Madaktari Bingwa.
Amewashukuru viongozi wa hospitali za Kanda ya Magharibi, madaktari wa Kanda ya Mbeya, na Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ushirikiano wao mkubwa katika kambi hiyo.
Kambi ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Kanda ya Magharibi inaratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni-Kigoma, Kitete-Tabora, na Katavi na imeanza rasmi Desemba 2, 2024 na inatarajiwa kumalizika Desemba 6, 2024.
#KAZIINAONGEA
0 Comments