Afrika Kuunganisha Nguvu Usambazaji Umeme


Afrika Kuunganisha Nguvu Usambazaji Umeme

Na Mwandishi wetu - Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema nchi za Afrika zinapaswa kuunganisha nguvu katika kuhakikisha wananchi wake wanafikiwa na nishati ya umeme ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akihutubia wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati unaoendelea jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema Tanzania imepiga hatua kwa  kusambaza umeme katika vijiji vyote na sasa inaweka mkazo katika kufikisha nishati hiyo ngazi ya vitongoji.

"'Mpaka sasa tumefanikiwa kuunganisha umeme katika vijiji vyote 12,318   na vitongoji 32,827 kazi inayoendelea ni kuunganisha umeme kwenye vitongoji 31,532 vilivyobakia kabla ya mwaka 2030" 

Rais Samia amesema kupitia mpango wa nishati Tanzania inafanya kazi ya kuongeza uzalishaji na uimarishaji wa miundombinu ya usambazaji wa umeme akiongeza kuwa nchi za Afrika lazima ziunganishe nguvu za wadau kwa lengo la kuwafikishia nishati ya umeme wananchi  milioni 300 kufikia 2030.

Aidha, amesema Tanzania inatekeleza mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia wenye lengo la kuwezesha wananchi wote kuondokana na madhara ya nishati ya kupikia isiyo safi kutoka asilimia 10 za sasa hadi 80 ifikapo mwaka 2030.

Aidha, Rais Samia amesema Tanzania ni kitovu cha kuuza nishati ya umeme kwa nchi zinazoizunguka zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya huku ikiendelea kuunganisha umeme kwa nchi za Zambia na Uganda.  

Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhutubia, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt Doto Biteko amesema Rais Samia amesimamia agenda ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha wananchi wanafikiwa na nishati ya umeme.

Amesema Tanzania imeongeza uzalishaji wa  umeme kutoka megawati 1,888 hadi 3,431.

Mkutano huo wa Wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati unahitimishwa leo Januari,2025.

Post a Comment

0 Comments