CHANGAMOTO ZA MAJI ZINAHITAJI USHIRIKIANO - SERIKALI


CHANGAMOTO ZA MAJI ZINAHITAJI USHIRIKIANO - SERIKALI

#KAZIINAONGEA

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imesema majibu ya changamoto zinazohusu maji na uondoshaji wa majitaka ni jukumu linalohitaji nguvu ya pamoja ya wadau wote wa maji ndani na jumuiya ya kimataifa. 

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango katika kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji, lililoandaliwa na Chuo cha Maji na kuanza Januari 29,2025 katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo la siku tatu kuanzia Januari 29 hadi 31, 2025 limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya maji wa ndani na nje ya nchi, ikiwa kauli mbiu ni “Majibu ya changamoto za maji na uondoaji wa majitaka katikati ya mabadiliko ya tabianchi”.


Dkt. Mpango amesema kuwa, kongamano hilo linapaswa kujadili namna ya kuhakikisha usalama na uendelevu wa rasilimali za maji, utupaji sahihi wa taka za sumu na hatarishi, kuweka mifumo endelevu ya kutenganisha aina mbalimbali za taka ngumu, matumizi ya maarifa asilia katika menejimenti ya rasilimali maji kama vile upandaji wa miti asilia rafiki wa maji katika maeneo ya vyanzo vya maji na ardhi oevu.

Pia amesisitiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayo rahisisha ushirikiano katika uendelezaji wa rasilimali maji. Aidha amewaalika watafiti na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kushirikiana na Serikali katika menejimenti ya rasilimali maji.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Chuo Cha Maji kimeendelea kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya maji nchini kupitia ufundishaji na uendelezaji wa wataalamu wa maji nchini pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu ikiwemo kufanya tafiti mbalimbali ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.


 Ameongeza kuwa, kongamano hilo ni sehemu ya kuimarisha upatikanaji wa mambo mapya ikiwemo ubunifu na mbinu za kushughulikia changamoto za maji na usafi wa mazingira nchini.

Awali Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam Karia amesema kumalizika kwa kongamano hilo kutawezesha kupatikana kwa ripoti maalum itakayotumika katika matumizi mbalimbali ya sekta ya maji na mazingira. Amesema kutokana na umuhimu wa kongamano hilo, Chuo kimedhamiria kufanyika kwa kongamano hilo kila mwaka ili kujadili mambo muhimu na kupelekea uelewa wa pamoja katika masuala yote yanayohusua maji na usafi wa mazingira.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments