CHUNYA YAPITISHA RASIMU YA BAJETI YA 38.7 BILION MWAKA 2025/26.
Mwandishi wetu, Mbeya
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imepitisha bajeti ya Sh 38.7 bilioni kwa ajili ya matumizi mbalimbali sambamba na kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya ,Bosco Mwanginde jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kupitia rasimu ya mapendekezo ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26.
Mwanginde amesema mbali na kupitisha rasimu hiyo pia wamejipanga kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani kutoka Sh 8.7 bilioni mpaka Sh 9 bilioni kwa mwaka 2025/26.
"Makusanyo hayo yametokana na vyanzo mbalimbali vya mapato hususani sekta ya madini,kilimo na nyinginezo sambamba na kubuni vyanzo vingine na usimamizi mzuri ya fedha ,"amesema.
Aidha amewataka madiwani kuendelea kuibua vyanzo vipya vya mapato sambamba na kuwashirikisha wananchi pindi wanapoibua miradi ili kuepuka kuitwisha mzigo serikali .
"Kuna miradi inaanzishwa bila utaratibu kama shule shikizi,vituo vya afya bila kushirikisha serikali au idara husika hali inayopelekea kushindwa kukamilika kwa wakati na kuwachonganisha wananchi na serikali.,"amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya ,Mbarak Batenga amewataka madiwani kushirikiana kikamilifu kuibua miradi mipya ili kuendelea kufanya vizuri katika makusanyo ya mapato ya ndani.
Batenga amepongeza usimamizi mzuri wa makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri na kupelekea kuongezeka kila mwaka na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayo elekezwa na serikali.
Sambamba na hilo amempongeza mwenyekiti wa halmashauri ,Bosco Mwanginde kwa kubuni chanzo kingine cha mapato ya uchimbaji wa madini ya Kopa katika Kata ya Mbugani
Ofisa mipango na uratibu Wilaya ya Chunya,Janeth Mwaigoga amesema kiasi cha Sh 669 milioni zimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake ,vijana na walemavu huku Sh 6.6 milioni kwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike zilizolewa kwa wanafunzi 3,300 wa shule za msingi na sekondari.
Mwisho.
0 Comments