DKT. BITEKO AZINDUA MKOPO WA BILIONI 100 KWA WASAMBAZAJI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


DKT. BITEKO AZINDUA MKOPO WA BILIONI 100 KWA WASAMBAZAJI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Mkopo wenye Riba ya asilimia 1% kwa mwezi (12% kwa mwaka), kwa mfumo wa reducing balance yenye riba halisi ya asilimia 6.6% ambapo Kiwango cha juu cha mkopo ni Shilingi Bilioni 1 kwa mfanyabiashara mmoja huku akisema ni hatua muhimu kuhakikisha Watanzania wanapata nishati salama na nafuu.

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ameongoza uzinduzi wa mpango mkubwa wa mikopo ya Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya kusaidia biashara na miradi ya kusambaza Nishati Safi ya kupikia nchini. Hafla hiyo imefanyika Januari 25, 2025 jijini Dar es Salaam, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wafanyabiashara, na wajasiriamali


Mpango huo, unaoratibiwa na Benki ya NMB, unalenga kuchochea matumizi ya Nishati Safi ya kupikia, hatua inayotilia mkazo afya, mazingira, na maendeleo ya kijamii. Akihutubia wadau waliokusanyika, Dkt. Biteko amesema:

“Mradi huu wa mikopo ni hatua muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata nishati salama na nafuu kwa matumizi ya nyumbani. Pia utachochea maendeleo ya sekta binafsi kupitia biashara za usambazaji wa mitungi na majiko ya gesi.”


Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, ameweka bayana masharti ya mkopo huu ni Riba ya asilimia 1% kwa mwezi (12% kwa mwaka), kwa mfumo wa reducing balance yenye riba halisi ya asilimia 6.6%., pili kiwango cha juu cha mkopo ni Shilingi Bilioni 1 kwa mfanyabiashara mmoja na sharti lingine ni Mkopo huu ni wa muda wa miaka miwili, ambapo mteja anaweza kuchagua muda unaomfaa lakini usiozidi miaka miwili.

Bi. Zaipuna pia ameeleza kuwa Benki ya NMB itatumia mpango wa "NMB Kijiji Day" kwa kushirikiana na kampuni ya Taifa Gas kutoa elimu ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia kwa vijiji 2,000 ifikapo mwaka 2025.


Katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, pia alitoa shukrani kwa Benki ya NMB kwa kujitokeza kusaidia maendeleo ya kijamii kupitia mikopo inayolenga kupunguza athari za matumizi ya nishati zisizo salama.

Wadau na wajasiriamali waliohudhuria walionesha matumaini makubwa juu ya mpango huu, wakibainisha kuwa utasaidia kuongeza ajira na kuboresha maisha ya Watanzania.


Mpango huu ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kuchochea matumizi ya gesi kama chanzo kikuu cha nishati safi, huku ukiwa na lengo la kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni, na hivyo kulinda mazingira.

Post a Comment

0 Comments