DKT. TULIA ATOA SARE KWA WANAFUNZI 3,000 MAZINGIRA MAGUMU


DKT. TULIA ATOA SARE KWA WANAFUNZI 3,000 MAZINGIRA MAGUMU

Mwandishi wetu, Mbeya

Taasisi ya Tulia Trust imetoa mahitaji na vifaa vya shule kwa wanafunzi 3,000 waishio mazingira magumu kutoka kata 36 na mitaa 181 katika Jiji la Mbeya.

Mahitahi hayo yamekabidhiwa jana Januari 17,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Kyela,  Josephine Manase kwa niaba ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa (Tamisemi ),Zainab Katimba  katika hafla iliyofanyika viwanja vya Ruanda Nzovwe.


Manase amesema serikali ya awamu ya sita inatambua mchango wa Taasisi ya Tulia Trust katika kuhudumia jamii sambamba na kutoa mahitaji kwa wazee wasio jiweza kwa kuwajengea makazi na kusaidia watoto wenye mazingira magumu.

"Tunatambua mchango wa Taasisi ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini,Dkt,Tulia Ackson kwa kugusa makundi mbalimbali katika jamii hususani kuwaendeleza vijana  20 wenye mazingira magumu nje ya nchi,"amesema.

Manase  amesema katika kuboresha sekta ya elimu Jiji la Mbeya,Serikali imetoa   Bilioni 23.4  kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 15 za msingi na miundombinu ya vyumba vya madarasa 280 kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kuhusu elimu bila malipo ,Manase amesema Serikali imetumia zaidi ya Sh 11.2 bilioni kuwekeza kwa wanafunzi 381,000 kwa Jiji la Mbeya lengo ni kuwezesha wanafunzi kupata elimu bora.


Mratibu wa masuala ya elimu kutoka Taasisi ya Tulia Trust ,Adili Kalinjila amesema huu ni msimu wa pili wa kutoa vifaa na kufanya idadi ya wanafunzi 6,000 wenye mazingira magumu kupata mahitaji ya shule zikiwepo sare na daftari.

"Mbali na kutoa mahitaji tutaanza programu ya kuwafuatilia mashuleni wanufaika wote kujua changamoto zao lengo ni kuwasaidia kutimiza ndoto zao za kupata elimu bora na kutimiza ndoto zao,"amesema.


Amesema lengo ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchangia elimu bila malipo kwa kuondoa vikwazo katika sekta ya elimu.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments