JIJI LA MBEYA LAJIPANGA KUFIKIA MAKUSANYO YA BILIONI 22 MAPATO YA NDANI
Mwandishi wetu, Mbeya
Halmashauri ya Jiji la Mbeya imejipanga kuongeza kukusanya kutoka Sh 19 bilioni mpaka zaidi ya Sh 22 bilioni kwa mwaka 2025/26 kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani .
Katibu Tawala Wilaya ya Mbeye,Mohammed Aziz amesema leo Alhamisi Januari 23,2025 kwenye kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mbeya (DCC) cha kupitia bajeti ya halmashauri ya Jiji.
Aziz ametoa kauli hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa na kwamba wamejipanga kuongeza ufanisi na ubunifu wa vyanzo vya mapato kwa kutumia mashine za poss kwenye maeneo ya masoko ,vituo vya mabasi .
"Katika makusanyo hayo asilimia 70 zitaelekezwa kwenye mikopo ya asilimia 10 ya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu sambamba na kutekeleza miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu,afya na minginezo,"amesema.
Amesema lengo ni kuiwezesha halmashauri kuongeza wigo wa kujitegemea kwa asilimia 21 kupitia mapato ya ndani na kufikia malengo yaliyo kusudiwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amesema ili kufikia malengo wameweka mikakati madhubuti ya kudhibiti mianya ya matumizi ya mabaya ya fedha na ubadhirifu wa miradi ya maendeleo.
"Lengo ni kuleta maendeleo ya pamoja sambamba na kudhibiti mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato kwa kuelekeza nguvu katika matumizi ya mashine za poss katika kila kata na kuibua vyanzo vipya vya mapato ,"amesema.
Aziz amesema ili kufikia malengo ya kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri kutoka Sh 19 bilioni kwa mwaka 2023/24 mpaka Sh 20 bilioni ni kuongeza wigo wa kushirikisha wadau hususani wa vyama vyama kwa kutoa ushauri na kuibua vyanzo vipya vya mapato.
Kaimu Mchumi wa Jiji la Mbeya ,Cosmass Kyovecho amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24 ,halmashauri ilikusudia kukusanya zaidi ya Sh 87.9 bilioni mpaka kufikia June 2024 ilikusanya zaidi ya Sh 93.7 sawa na asilimia 107.
Amesema kwa mwaka 2024/25 walikusudia kukusanya kiasi cha Sh 97.5 bilioni na mpaka kufikia Desemba mwaka jana walikusanya zaidi ya Sh 52.9 bilioni huku kukiwa na mikakati zaidi ya kutanua wigo wa kuongeza vyanzo vipya vya mapato.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya,Dour mohamed Issa amesema kuwa bajeti yao imejikita kuhudumia wananchi katika kuleta maendeleo
"Mbeya hatuijengi peke yetu hivyo tunaomba washiriki kutoa maono yenu katika bajeti ili kuleta chachu ya maendeleo katika Jiji letu,"amesema.
Mwandishi wetu-Mbeya
0 Comments