MAAGIZO YA RAIS DKT. SAMIA KUHUSU MATUMIZI YA MFUMO WA TMX YALIVYOCHANGIA UWAZI KWENYE MINADA YA MAZAO MSIMU 2024/2025


MAAGIZO YA RAIS DKT. SAMIA KUHUSU MATUMIZI YA MFUMO WA TMX YALIVYOCHANGIA UWAZI KWENYE MINADA YA MAZAO MSIMU 2024/2025

Mwandishi wetu, Mtwara

Msimu wa uuzaji na ununuzi wa mazao ya Biashara hapa nchini hatimaye umefikia mwishoni huku kukiwa na mafanikio makubwa kwa wakulima kutokana na bei za kuridhisha zilizofikiwa kupitia minada iliyofanyika katika maeneo mbalimbali.

Minada ya msimu 2024/2025 iliratibiwa na kuendeshwa kwa usimamizi wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) chini ya Wizara ya Fedha, ikishirikiana na Bodi za Mazao mbalimbali, Vyama Vikuu vya Ushirika, Bodi ya Usimamizi wa Maghala, Wizara Kilimo na wadau wengine katika sekta ya Kilimo Nchini.

Baadhi ya mazao ambayo Minada yake iliendeshwa na TMX ni Kakao, Ufuta, Mbaazi, Kahawa, Dengu, Soya, Chai na Korosho ambayo kwa mara ya kwanza iliuzwa kupitia soko hilo la Bidhaa kwa asilimia 100 huku bei yake ya juu ikifiskia shilingi 4,195/= kwa Kilo Moja na kuweka historia ambayo haijawahi kufikiwa.

Uingizwaji wa mauzo ya Korosho katika mfumo wa TMX ulisikumwa na juhudi za Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alitamani kuona minada ikifanyika kwa uwazi kupitia njia za kisasa (Online), ili kuongeza ushindani kwa Wanunuzi na kuchangamsha soko ili kuweza kumnufaisha Mkulima.

Kuelekea Msimu wa Korosho 2024/2025, Mhe.Rais Dkt.Samia alisisitiza juu ya TMX kuhusika moja kwa moja katika usimamizi wa wa Minada kwa lengo la kuhakikisha kuwa biashara ya zao hilo inafanyika kwa uwazi na kunufaisha wakulima ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamika kutokutendewa haki wakati wa mauzo.

“Nisisitize matumizi ya mifumo ya Stakabadhi Ghalani na TMX, ndio utakuwa muelekeo wetu wetu, muelekeo wa Nchi hii katika muelekeo wa mazao ya kilimo, ili tumpe mkulima faida ya jasho lake mifumo hii ndio inayokwenda kumnufaisha mkulima, lengo letu pia ni kutaka kupata takwimu sahihi za kilimo katika Taifa letu ili tuweze kuziweka kimataifa na Tanzania isomeke vyema kwenye ramani ya biashara ya Kilimo” Mhe.Rais Dkt. Samia September 2024.


Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX Ndg. Godfrey Malekano, Msimu wa Korosho 2024/2025 ulikuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya Tani 400,008 ziliweza kuuzwa kupitia katika Mikoa mitano ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Morogoro na kuingiza kiasi cha fedha zaidi ya Shilingi Trilioni 1.3.

Kwa upande wa zao la Ufuta Msimu 2024/2025 Malekano anaeleza kuwa Soko la Bidhaa Tanzania liliuza Tani 144,000 na Mbaazi Tani 100,000 na kwa upande wa Kakao TMX iliuza Tani 12,000 na Dengu Tani 21,000 kikiwa ni kiasi kikubwa zaidi kuwahi kufikiwa ikilinganishwa na misimu ya mazao iliyopita.

“Kupitia mfumo huu, na usimamizi wa wazi wa mauzo katika mazao yaliyotajwa wanunuzi walipata bidhaa kwa wakati na uhakika, na walilipa fedha kwenda kwa wauzaji (wakulima) ambao nao walipokea malipo yao kwa wakati” 

“Tumshukuru sana Mhe. Rais Dkt.Samia kwani amehusika kwa kiasi kikubwa sana kwenye kufanikisha hiki kilichotokea kupitia maelekezo na maagizo yake ambayo sisi kama watendaji tuliyachukua na kuyasimamia kwa ufanisi mkubwa na matokeo yake ndio haya ambayo yameonekana mwisho wa msimu wa mazao mbalimbali” amesisitiza Malekano

Bodi ya Korosho Tanzania ndio msimamizi mkuu wa Tasnia ya Korosho nchini, na kupitia taarifa yake rasmi inaeleza kuwa kiasi cha fedha kilicholipwa kwa wakulima wa Korosho katika msimu 2024/2025 ni kikubwa ikilinganishwa na msimu 2023/2024

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Ndg. Francis Alfred, Wakulima wa korosho wamelipwa zaidi ya Shilingi Trilioni 1.46 katika Msimu wa korosho 2024/2025 ikilinganishwa na Bilioni 500 walizolipwa katika msimu uliopita wa 2023/2023 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Bilioni 540.

“Mafanikio haya ya msimu 2024/2025 yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali hususan kwenye eneo la uwazi katika minada, sisi kama wasimamizi wakuu wa Tasnia jukumu letu ni kuwezesha wadau wengine kutekeleza wajibu wao bila vikwazo na hilo kwakweli tumelifanya na tutaendelea kulifanya”

Hivyo ndivyo Msimu wa Mazao ya Bishara 2024/2025 ulivyohitimishwa huku Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ikiendelea kuweka mikakati zaidi ya kuhakikisha kuwa kunakuwa na muendelezo wa usimamizi mzuri wa uuzaji na ununuzi wa mazao hayo katika misimu ijayo, kwa lengo la kuendelea kumnufaisha mkulima na Taifa kwa ujumla

Post a Comment

0 Comments