MTEULE WA RAIS SAMIA AAPISHWA MANYARA

 


MTEULE WA RAIS SAMIA AAPISHWA MANYARA

#KAZIINAONGEA

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga amemuapisha Michael John Semindu

Mkuu wa wilaya ya Mbulu baada ya kuteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Januari 25, 2025 kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.

Hafla ya uapisho huo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara mjini Babati, huku viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya siasa na wa dini wakihudhuria.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa tukio la uapisho huo, Mkuu wa Mkoa Manyara amempongeza Mkuu mpya wa Wilaya ya Mbulu na kumshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza nguvu kazi ya watendaji katika Mkoa wa Manyara.


Aidha Sendiga amewainishia wakuu wa wilaya waliopo katika mkoa wake, vipaumbele vya mkoa ili kufikia malengo ya pamoja ambavyo ni ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kuwahudumia Wananchi wa Manyara na kuleta maendeleo katika Taifa, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kuanzia ngazi ya mtaa mpaka katika Halmashauri zao kwa wakati, kusimamia ulinzi na usalama kwa kuweka mikakati ya kudhibiti uhalifu, kusimamia usafi wa mazingira ili kuweka mkoa katika hali ya usafi pamoja na usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.  

Pia, ameongeza kwa kusema, "natambua kuwa kila mmoja amejiwekea vipaumbele vyake kama Mkuu wa Wilaya husika, hivyo kama Mkoa pia una vipaumbele vyake ambavyo kila mmoja anatakiwa kuvielewa na hatimaye kuweza kuvitekeleza,

 “Naomba nendeni mkatimize wajibu wenu ipasavyo na mkatekeleze matarajio chanya ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwani amewaamini na ndio maana amewapa nafasi hizo, hivyo ukiaminiwa, nawe unatakiwa ujiaminishe ili kuweza kutimiza adhima hii kikamilifu.” amesema Sendiga.


Akizungumza mara baada ya kuapishwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Michael John Semindu ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wenzake pamoja na kuyapokea maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuyatekeleza majukumu yao yote kwa weledi mkubwa.

" Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyemuwezesha Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuniona na kuniteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, si kwamba mimi ni bora sana kuliko wengine laa hasha! isipokua ni wakati wa Mungu umefika wa mimi kuonekana katika nafasi hii, hivyo nitatekeleza yote aliyoniagiza Mkuu wangu wa Mkoa " amesema Semindu.


Ikumbukwe kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Semindu kabla ya kuteuliwa na Rais Dkt. Samia kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, alikuwa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments