SERIKALI KUIMARISHA TAFITI KATIKA KILIMO


SERIKALI KUIMARISHA TAFITI KATIKA KILIMO

Lengo ni kuendelea kuwa tegemeo katika uzalishaji chakula Afrika

#KAZIINAONGEA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewaeleza Wakuu wa Nchi na Serikali Barani Afrika kuwa, Tanzania itaendelea kuimarisha masuala ya utafiti na kushirikisha Sekta binafsi, Taasisi za Umma zinazojishughulisha na kilimo ili kuhakikisha nchi inakuwa tegemeo katika uzalishaji wa chakula Barani Afrika.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo, alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika, kupitisha Programu ya Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (CAADP 2026 - 2035) uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha Speke Resort, Munyonyo, Kampala nchini Uganda.

Majaliwa amesema, viongozi wa nchi za Afrika wameonesha matumaini makubwa na mikakati iliyowekwa na Tanzania katika kuzalisha mazao ya chakula yenye ubora hasa mpunga na mahindi, akitaja kuwa ni mafanikio makubwa katika Sekta ya Kilimo nchini.

Majaliwa amesema kuwa, Tanzania imeweka mkakati wa kuhakikisha inaendelea kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuza ziada nje.


Naye, Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza ili kuongeza tija na kukuza ajira hususan kwa vijana.

“Natamani watu washindane kwa ubora katika uzalishaji, mfano mchele wa kutoka Tanzania ni bora zaidi na gharama yake ipo chini, kuna wakati walitaka nizuie usije lakini nikawataka nao wajitahidi kushindana katika uzalishaji wa bidhaa zenye ubora,” amesema Rais Museveni.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments