SERIKALI KUTOA KINGATIBA YA MATENDE NA MABUSHA
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongoza na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatarajia kuanza zoezi la umezeshaji wa Kingatiba dhidi ya magonjwa ya matende na mabusha au Ngirimaji kwa Wananchi waliopo kwenye Kata kumi za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia Januari 22 hadi 26, 2025, ambapo Kata hizo zinaelezwa kuwa na maambukizi makubwa ya ugonjwa huo.
Kutolewa kwa chanjo hizo ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia, katika kuhakikisha Wananchi wanaepuka kupata ugonjwa huo.
Hayo yamebainishwa Januari 15, 2025 kwenye kikao cha Kamati ya Afya ngazi ya msingi kilicholenga kuweka mikakati ya kuanza kwa zoezi la umezeshaji wa kingatiba hizo kwa wananchi, kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa, Kata ambazo zinatarajiwa kufikiwa na zoezi hili ni pamoja na Kijitonyama, Makumbusho, Kigogo, Ndugumbi, Hananasifu, Mzimuni, Tandale, Kinondoni, Magomeni na Mwananyamala ambapo zoezi hili limelenga kuwafikia watu zaidi ya 284,035.
“Wapo watu ambao tunaishi nao kwenye maeneo yetu bado wanasumbuliwa na mabusha na matende, huu ni ugonjwa mbaya na unaathiri shughuli za kijamii na uchumi wa familia zetu,” amesema Mtambule.
Mtambule amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa Sekta kwa kuendelea kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za tiba na kinga nchini, ikiwemo kutoa kingatiba hizo za ugonjwa wa matende na mabusha katika Wilaya ya Kinondoni na kuitaka Kamati ya Afya ngazi ya Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kumeza kingatiba hizo ili waweze kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha huku akitoa onyo kali kwa wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya kuhujumu zoezi hilo kwa kuwahadaa wananchi na taarifa za uongo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Peter Nsanya amesema kuwa, Halmashauri inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na makundi maalumu juu ya umuhimu wa kingatiba hizo na kwamba, zaidi ya wahudumu wa afya 146 wanaendelea na kazi ya kutoa elimu kwa wananchi na walengwa watakaomeza kingatiba hizo ni watu wote wenye umri kuanzia miaka mitano (5) na kuendelea, huku huduma zitatolewa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, wagawa dawa na walimu waliopewa mafunzo ya jinsi ya kugawa dawa hizo.
Zoezi la ugawaji wa Kingatiba hizo litafanyika kwa kupitia nyumba kwa nyumba kwenye makazi yetu, shuleni,ofisi za umma na binafsi,vituo vya kutolea huduma za afya,vituo vya usafiri, sokoni na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments