SERIKALI KUTUMIA BIL.38.3 UJENZI WA BARABARA RUVUMA


SERIKALI KUTUMIA BIL.38.3 UJENZI WA BARABARA RUVUMA

#KAZIINAONGEA

Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Mkoa wa Ruvuma, kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imeidhinisha Shilingi Bilioni 38.394, kwa ajili ya kufanya matengenezo na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,145, madaraja madogo 50 na makalavati 57, Mkoani Ruvuma.

Hatua hiyo ya utoaji fedha, ni muendelezo wa Miradi ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia, katika kuhakikisha huduma mbalimbali zinawafikia Wananchi katika Sekta zote.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Silvester Chinengo, ametoa ufafanuzi kuhusiana na Mradi huo, wakati akitambulisha barabara mpya mbili ya Muungano-Majengo na barabara ya Kilimo Mseto-Pm House, na kusema kuwa, ujenzi wa barabara ya kwanza yenye urefu wa kilometa 1.5, itagharimu kiasi cha Shilingi Milioni 949 pamoja na barabara ya Mjimwema-Mkuzo yenye urefu wa kilometa 1.1 ambayo ujenzi wake umegharimu Shilingi Milioni 426.

Amesema, kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 7.8 ni bajeti ya barabara kuu, Shilingi Bilioni 9.8 zinatokana na tozo ya mafuta, Shilingi Bilioni 4.5 fedha kutoka mfuko wa Jimbo na Shilingi Bilioni 16.2 ni fedha za Mradi wa Agricconect chini ya Umoja wa Ulaya(EU).

“Barabara hizi zimejengwa kutokana na fedha za tozo ya mafuta na zimeleta mabadiliko makubwa kwenye mitaa kwa sababu wakati wa mvua wananchi waliathirika na mafuriko pamoja na matope, kwa sasa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa mitaa hiyo na mali zao, pia zitarahisisha sana shughuli za usafiri na usafirisha kwa wananchi wa maeneo hayo,” amesema Chinengo.

TARURA Mkoa wa Ruvuma inahudumia mtandao wa barabara wa kilometa 71,146.21, madaraja 306, makalavati 531, drifti 14 na mitaro yenye urefu wa kilometa 6.91 ambapo kilometa 2,312 sawa na asilimia 32.36 ni za mjazio, kilometa 3,873.85 sawa na asilimia 54.12 ni za mkusanyo na kilometa 959.52 sawa na asilimia 13.43 ni za jamii, na kwamba, katika barabara hizo kilometa 128.66 sawa na asilimia 1.8 ni za lami na zege, kilometa 1,429 sawa na asilimia 20 za changarawe na kilometa 5,588 sawa na asilimia 78.2 za udongo.

Akizungumzia miradi viporo amesema, kuna mradi mmoja wa kuondoa vikwazo vya usafirishaji (RISE) unaotekelezwa kwenye Halmashauri ya Madaba, Mbinga Mji, Halmashauri ya Wilaya Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru ambapo Serikali imetenga Shilingi Bilioni 2.28 kwa ajili ya kuondoa vikwazo barabarani ikiwemo kujenga madaraja na barabara za changarawe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia zaidi ya 70.

Chinengo, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuongeza bajeti ya barabara kwa kuingizwa vyanzo vipya vya mfuko wa Jimbo na Tozo, kwani awali walikuwa na bajeti moja kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara  pia vimewezesha kuongezeka kwa mtandao wa barabara ambapo zaidi ya asilimia 65 zinapitika majira yote ya mwaka, kuongeza mtandao wa barabara za lami na ufungaji wa taa katika Makao Makuu ya Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea Godfrey Mngale alieleza kuwa, katika barabara ya Mjimwema-Mkuzo kazi zilizofanyika hadi sasa ni kuweka tabaka la lami, kujenga mitaro ya kupitisha maji kwa kutumia mawe pande zote mbili.

Amesema, ujenzi wa barabara hiyo umewezesha kubadilisha mazingira ya maeneo hayo pamoja na kupandisha thamani ya viwanja na vyumba mbapo awali wananchi wa maeneo hayo walipata adha kubwa hasa wakati wa mvua kutokana na utelezi kwa kuwa eneo hilo lina mteremko mkali na amewataka wananchi waliopitiwa na barabara hiyo, kuhakikisha wanalinda miundombinu ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa kuwa waliteseka kwa muda mrefu kabla Serikali kupitia TARURA kuimarisha barabara kwa kiwango cha lami.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments