SERIKALI KUTUMIA FURSA YA MKUTANO NISHATI SAFI KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII


SERIKALI KUTUMIA FURSA YA MKUTANO NISHATI SAFI KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII 

#KAZIINAONGEA

Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imejidhatiti kwa kutangaza Vivutio vya Utalii kwa kutumia fursa ya Mkutano wa Afrika wa Nishati unaotarajiwa kuanza Januari 27, 2025, Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas akizungumza Januari 26, 2025, alibainisha kuwa, maandalizi yamekamilika kwa kuhakikisha Vivutio vya Utalii vinawasilishwa vyema kwa wageni wa mkutano huo wa Kimataifa.


Dkt. Abbas akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu (Utalii) Nkoba Mabula, Mkurugenzi Mkuu wa TTB Ephraim Mafuru, na Viongozi wengine Waandamizi, ametembelea maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuvutia wageni, yakiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1, 2, na 3), pamoja na maeneo ya Ocean Road na Aga Khan.

“Kila eneo tumelipambwa kwa taswira halisi za Utalii wetu, zikiwemo ngozi za wanyama na picha za mandhari ya kuvutia, ili kuwapa wageni taswira ya kile ambacho nchi yetu inatoa katika Sekta ya Utalii na Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tayari imeandaa safari za wageni kwenda maeneo ya vivutio vya utalii," amesema Dkt. Abbas.

“Kuna maafisa Waandamizi wa Benki ya Dunia wanaotarajia kutembelea Serengeti, na tunaendelea kuratibu ziara za wageni wengine wengi, Tanzania iko tayari kuwakaribisha wote,” ameongeza.


Mkutano wa Africa Energy Summit umevutia viongozi Waandamizi, Wawekezaji, na washiriki kutoka Mataifa mbalimbali, na ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kujitangaza Kimataifa siyo tu kama kitovu cha Nishati, bali pia kama mahali pa kipekee kwa utalii wa kipeo cha juu.   

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments