SERIKALI YAENDELEA NA UKAMILISHAJI TARATIBU ZA MFUKO NISHATI SAFI YA KUPIKIA
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanzisha Mfuko wa Nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis ameiarifu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira 16, Januari, 2025 Jijini Dodoma, alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyotokana na taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati iliyowasilishwa Bungeni Februari, 2024.
Amesema Kanuni za Usimamizi wa miradi ya biashara ya kaboni zimebainisha ruzuku kupitia hakimiliki za kaboni zinazopatikana kutokana na kupunguza matumizi ya nishati inayochafua mazingira, hivyo ruzuku hii ni sehemu ya juhudi za Kitaifa za kutekeleza malengo ya kupunguza gharama kwa watumiaji wa Nishati safi.
Khamisi ameileza Kamati hiyo kuwa, katika jitihada za kupunguza gharama za matumizi ya Nishati mbadala, Serikali imesaini makubaliano ya awali na Uwekezaji kuhusu ruzuku ya Shilingi Bilioni 8.64 kwenye Nishati safi ya kupikia mbapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku.
Aidha, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya Nishati mbadala kwa njia mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma kupitia Vyombo vya Habari, ziara za viongozi.
Ameendelea kusema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kuhamasisha na kuhimiza Halmashauri zote za vijiji kuainisha misitu yote ya vijiji yenye sifa ya kuingizwa kwenye mpango wa Biashara ya Kaboni.
Amefafanua kuwa, uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa biashara ya kaboni katika kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato kwa jamii unaendelea kutolewa kwa wananchi ambapo Serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa mikataba ya biashara ya kaboni inanufaisha wananchi na inafanyika kwa mujibu wa Kanuni za usimamizi wa biashara ya kaboni.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments