SERIKALI YAFANYA MAANDALIZI YA UJENZI WA MTANDAO WA MAJI WA TAIFA
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi wa mtandao wa Maji wa Taifa (National Water Grid) na hivyo kuifanya Tanzania kuyafikia maeneo mengi zaidi katika huduma ya maji na kusukuma mbele maendeleo ya Taifa.
Akizungumzia mkakati huo, wakati wa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika (African Ministers’ Council on Water-AMCOW), Dkt. Rashid Mbaziira, katika Ofisi za Wizara ya Maji, Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Menejimenti ya Wizara, Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amesema kuwa, Serikali ya Rais Samia, ipo katika maandalizi hayo, kwa lengo la kuboresha huduma ya maji nchini.
Mazungumzo hayo yamehusu Maandalizi ya Dira ya Maji ya Afrika (Africa Water Vision 2050), pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika Kanda ya Afrika Mashariki ambao unatarajia kufanyika Machi 4-7, 2025.
“Niwaombe AMCOW mtuunge mkono katika eneo hili, pia muendelea kuungana na Tanzania katika utekelezaji wa programu mbalimbali zinazohusisha usimamizi na uendelezaji wa Rasilimali za maji, ujenzi wa miradi ya maji na usambazaji maji,”amesisitiza Waziri Aweso.
Katibu Mtendaji, Dkt. Mbaziira, ameishukuru Serikali ya Tanzania kutokana na ushirikiano mzuri kwamba, Tanzania ambayo ni mwanachama wa AMCOW itashika nafasi ya Makamu wa Rais wa AMCOW Kanda ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi za Tanzania, Burundi, Djibuti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini na Uganda mwezi Februari 2025 na kwamba hakuna mashaka na utayari wa Serikali ya Tanzania na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika maeneo mbalimbali kwani anajua maji ni uhai na ni nyenzo muhimu katika kusukuma maendeleo ya Sekta mbalimbali katika jamii.
Aweso amemshukuru Katibu Mtendaji na kuahidi ushirikiano wa kutosha kutoka Tanzania katika utekelezaji wa maagizo yote ambayo yamekuwa yakitolewa na Baraza hilo la mawaziri na kwamba tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani ameonesha nia ya dhati ya kuhakikisha Sekta ya Maji inapiga hatua.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments