SERIKALI YAITAKA BODI YA BIMA YA AFYA (NHIF) KUHAKIKISHA WATUMIAJI MFUKO HUO WANAPATA HUDUMA BORA ZA AFYA
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya, imetoa rai kwa Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuangalia namna bora itakayowezesha Mfuko kutatua changamoto zote za upatikanaji wa vifaa tiba kwa haraka kwa kushirikiana na wadau ili Wanachama wa Mfuko huo, wasighadhibike kwa namna yeyote wanapohitaji huduma bora kutoka kwenye Vituo vya Afya.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama ameyasema hayo Jijini Dodoma Januari 21,2025 wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo amesema kuwa, matamanio yake ni kuwa zile huduma zote za msingi zipatikane kwenye Bima ya Afya kwa wote.
"Sasa niendelee kutoa Rai kwa wajumbe wa Bodi kuangalia namna bora itakayowezesha mfuko kuhakikisha changamoto zote zinazotokana na upatikanaji wa vifaa tiba zinatatuliwa kwa haraka sana kwa kushirikiana na wadau watoa huduma za afya ili wanachama wetu wasighadhibike kwa namna yeyote wanapohitaji huduma zilizo bora kutoka kwenye vituo vyetu wanavyotolea huduma za afya," amesisitiza.
Awali akitoa salamu Dkt Baghayo Saqware ambaye ni Kamishna wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ameleeza kuwa, wanufaika wa Bima za Afya na Bima zingine, wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2021 wanufaika walikuwa Milioni 14.2 na mwaka 2022 Milioni 17.8 huku mwaka 2023 walifikia Milioni 23 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 29 kila mwaka.
"Ukijumlisha Bima za Afya na Bima zingine wanufaika wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka, mwaka 2021 tulikuwa na wanufaika Milioni 14.2 wakati mwaka 2022 walikuwa Milioni 17.8 na mwaka 2023 wamefikia Milioni 23, hili ni ongezeko la wastani wa asilimia 29 kwa mwaka na hii inatokana na Sera nzuri na maelekezo mazuri kutoka kwenye Wizara zetu za Kisekta na Wizara ya afya," amesema Dkt. Saqware
Kwa upande wake Dkt Irene Isaka ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mbali na kueleza mafanikio ya Bodi iliyomaliza muda wake kuwa waliweza kuongeza wigo wa wanufaika wa Bima ya Afya kwa kusimamia usajili wa wanachama lakini amekiri kuwa, walikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa gharama za magonjwa yasiyoambukiza, Uhiari wa wananchi kujiunga kwenye Mfuko wa Bima ya Afya na kukosekana kwa Mfumo madhubuti wa Rufaa ya wagonjwa nchini.
"Bodi iliyomaliza muda wake ilikuwa na changamoto kadhaa, mojawapo ni kuongezeka kwa gharama za magonjwa yasiyoambukiza, kukosekana na utamaduni kuwa na Bima kwa wananchi kabla ya kujiunga, Uhiari wa wananchi kujiunga kwenye Mfuko wa Bima ya Afya, kuchelewa kulipwa kwa fedha ambazo mfuko uliikopesha Serikali, kukosekana kwa mfumo madhubuti wa Rufaa ya wagonjwa nchini," ameeleza.
"Vilevile walifanikiwa kuongeza wigo wa wanufaika wa Bima ya Afya kwa kusimamia usajili wa wanachama ambapo kutoka Milioni 1,212,519 mwaka 2020 hadi kufikia Milioni 1,246,046 Machi 2024 sawa na ongezeko la asilimia tatu," amesisitiza.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments