SERIKALI YAKABIDHI MILIONI 528 KWA VIKUNDI 52 IRINGA
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, imeanza rasmi zoezi la utoaji mikopo kwa wanufaika 52 wa vikundi vya Vijana, Wanawake na wenye Ulemavu.
Zoezi hilo limeshuhudiwa na Mkuu wa wilaya ya Iringa Kheri James ambae amevikabidhi vikundi 52 vilivyo kidhi vigezo, hundi ya shilingi 528,764,660 ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya Uwezeshaji wa Wananchi kiuchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo Kheri James ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kutimiza wajibu huo wa kisheria wenye lengo la kuinua hali za kiuchumi za wananchi hasa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.
Ameeleza kuwa lengo la utoaji wa mikopo hiyo ni kuunga mkono juhudi za Wananchi katika shughuli zao za uzalishaji mali, kuongeza mnyororo wa thamani, kutengeneza ajira, kukuza biashara na kuchochea upatikanaji wa huduma katika jamii. Hivyo amewataka Wananchi kuitumia vyema mikopo hiyo.
Pamoja na mambo mengine Mkuu wa wilaya amewahimiza wana vikundi wote kuchapa kazi kwa uaminifu na ubunifu ili kuongeza uzalishaji na kujenga mshikamano miongoni mwao.
Serikali wilayani Iringa tayari imefanikiwa kutoa mikopo katika Halmashauri zake mbili na inaendelea kutoa.
*#KAZIINAONGEA
0 Comments