SERIKALI YAKUSANYA MAONI YA WADAU KUBORESHA MIFUMO YA KODI


SERIKALI YAKUSANYA MAONI YA WADAU KUBORESHA MIFUMO YA KODI

#KAZIINAONGEA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea na mchakato wa ukusanyaji maoni kwa Wadau mbalimbali ili kuboresha mabadiliko ya mifumo ya kodi kwa namna itakayowafaidisha Wananchi na nchi kwa ujumla.

Mkutano huo wa wadau wa kodi, umefanyika 17, Januari, 2025, katika ukumbi wa Lyakale Mjini Shinyanga, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi ambapo amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika michakato ya kuboresha mifumo ya kodi, akisema kuwa michango na maoni yao ni muhimu na itatumika kama sehemu ya mikakati ya kuleta mageuzi ya kimsingi katika Sekta ya kodi.

“Rais Dkt. Samia ni Mwanamapinduzi wa kweli, anayehamasisha na kusikiliza maoni ya wananchi, anachukua hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa maoni ya wananchi yanatekelezwa kwa manufaa ya wengi, Tume hii ya Rais haiachi jambo lolote nyuma, inazingatia taaluma na weledi wa hali ya juu katika kufanya tathmini ya mifumo ya kodi, hivyo, michango yenu inachukuliwa kama maoni muhimu kwa kuboresha mifumo ya kodi na itafanyiwa kazi,” amesema Wakili Mtatiro

Amesema, mkutano huu ni sehemu ya juhudi za Tume ya Rais Samia ya uboreshaji wa mifumo ya Kodi ambayo imefanya mkutano na wadau hao wa masuala ya kodi, kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu uzoefu, changamoto na mapendekezo ya namna ya kuboresha mifumo ya kodi nchini, changamoto za kodi na kwamba changamoto za kodi niza Kitaifa na ameahidi, Serikali kuendelea kuboresha mifumo ili kuhakikisha, masuala ya kodi yanakuwa endelevu na yanahusisha pande zote kwa faida ya nchi nzima.

Naye, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya uboreshaji wa Kodi, CPA Leonard Mususa, ameeleza kuwa, Tume hiyo inaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu mifumo ya kodi, mapato na tozo mbalimbali zinazohusiana na Sekta ya kodi.

CPA Mususa amesema, kazi hii inaimarisha juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa mfumo wa kodi unakuwa rafiki kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, na kwamba Tume inashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa, kodi zinakusanywa kwa njia bora na yenye haki, huku ikifanya mabadiliko ili kuondoa kero na malalamiko ambayo yamekuwa yakichochea malumbano.

“Tume ya Rais inatekeleza majukumu yake kwa umakini mkubwa ili kuondoa kero za kodi na kuboresha mazingira ya biashara na Uwekezaji, na imelenga kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi na kwa upande mwingine, tunafanya tathmini ya kina ili kuona ni hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa ili kuboresha mifumo ya kodi nchini,” ameeleza CPA Mususa.

Mkutano huo umetoa fursa kwa wadau muhimu wa masuala ya kodi wa Mkoa wa Shinyanga kutoa maoni yao kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika masuala ya kodi ambapo pia wamependekeza njia mbalimbali za kutatua changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu katika ukusanyaji wa kodi, kuboresha mawasiliano kati ya Serikali na wafanyabiashara na kuongeza ufanisi katika utendaji wa mifumo ya kodi.

#KAZIINAONGEA

Post a Comment

0 Comments