SERIKALI YAPONGEZWA KUWA KINARA WA AMANI,USALAMA UKANDA WA MAZIWA MAKUU
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongezwa kwa kuwa kinara katika masuala mbalimbali yanayolenga kuleta amani na usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya katika Ukanda wa Maziwa Makuu Bw. Johan Borgstam hivi karibuni Jijini Dodoma, ambaye yupo katika ziara ya kikazi ambapo kwa nyakati tofauti, amefanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Cosato Chumi, alimwakilisha Waziri Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, mazungumzo yaliyokita kujadili masuala ya ulinzi na usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Katika mazungumzo na viongozi hao Bw. Borgastam ameeleza kuwa, Umoja wa Ulaya unatambua na kuthamini mchango wa kipekee unaotolewa na Tanzania katika kuleta amani na usalama wa kudumu katika Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu zinazokabiliwa na changamoto za kisiasa ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.
Borgastan ameongeza kuwa, ziara yake hapa nchini inalenga kupata na kubadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu masuala ya usalama na amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu, kwa kuwa daima Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuendesha operasheni mbalimbali na majadiliano ya kuleta ufumbuzi wa kudumu juu ya changamoto za kisiasa zinazokabili Ukanda huo.
Aidha, amesema kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo Tanzania katika kuleta amani na usalama Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kwa upande wao Viongozi wa Tanzania, wameushukuru Umoja wa Ulaya kwa mchango wake wa aina mbalimbali wanaoendelea kutoa katika kuhakikisha Ukanda wa Maziwa Makuu, unakuwa na amani ya kudumu ili wananchi wake wawe huru kuendesha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa mustakabali mwema wa kizazi cha sasa na kijacho.
Ukanda wa Maziwa Makuu una jumla ya Nchi Wanachama 12, ambao ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, DRC, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda na Zambia.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments