SERIKALI YASISITIZA TAFITI ZAIDI KATIKA RASILIMALI MAJI
#KAZIINAONGEA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema tafiti zinahitajika zaidi katika menejimenti ya rasilimali maji ili kuwezesha maarifa mapya na uelewa mpana kuhusu upatikanaji na ubora wa maji.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam Januari 29,2025.
Dkt. Mpango amesema ni muhimu tafiti kuelekezwa kujibu changamoto zinazokabili menejimenti ya rasilimali za maji hususani kubaini, kuotesha na kutunza miti ya asili ambayo inafahamika katika maeneo mbalimbali ya kila wilaya au mikoa nchini kuwa ni rafiki wa maji.
Vilevile amesisitiza umuhimu wa tafiti hizo kuangazia teknolojia rahisi, endelevu na ya gharama nafuu ya kuvuna maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, sambamba na uchimbaji wa mabwawa, na kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua yanayotiririka kwa ajili ya umwagiliaji wa mashamba na kukidhi mahitaji ya mifugo,
Kadhalika, umuhimu wa kuangazia tafiti zitakazokuza kilimo janja namna bora ya kurejesha uasili wa maeneo yaliyoharibiwa na mmomonyoko wa udongo na ukame wa muda mrefu, kubuni mifumo, mbinu na hata motisha ya kutunza vyanzo vya maji na ardhi pevu pamoja na kuwianisha matumizi ya maji kwa binadamu, mifugo na wanyamapori.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa Kongamano hilo kuangazia suala la kubuni mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za uondoshaji majitaka kwa wote na kutoa kipaumbele kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi.
Ameongeza kuwa, suala hilo linapaswa kuhakikisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi yanajumuishwa katika mipango ya kila nchi ili kuendeleza matumizi bora ya maji na mifumo ya uondoaji wa majitaka pamoja na kujenga uwezo wa jamii kutambua, kuhimili na kukabiliana na matukio ya hali mbaya ya hewa.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments