#KAZIINAONGEA
Katika kuhakikisha uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja unakuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefungua milango ya fursa ya uwekezaji wa ubia kati ya wananchi na serikali kwenye fainali za CHAN 2025 na AFCON 2027.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, hivi karibuni alipofungua kikao maalum cha kujadili fursa za kiuchumi na maandalizi kuelekea mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika nchini yakizihusisha pia nchi za Kenya na Uganda.
Katika kikao hicho, Dkt. Biteko amebainisha kuwa maandalizi ya mashindano hayo ni fursa adhimu ya kuimarisha miundombinu na kuongeza ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa uwekezaji kwa njia ya ubia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia (PPPC), David Kafulila, amesema kuwa mfumo wa Ubia (PPP) ni njia bora ya kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali huku ukileta uzoefu, teknolojia, na ufanisi wa kuendesha miradi mbalimbali.
“Ubia ni fursa kubwa. Tunatoa wito kwa mamlaka za serikali kutangaza maeneo yenye fursa za uwekezaji na kuwakaribisha wawekezaji, hasa tunapoelekea mashindano ya AFCON 2027,” amesema Kafulila.
Kwa mujibu wa Kafulila, ziara maalum ya wataalamu wa PPPC katika Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, zikiwemo Temeke, Ilala, Kinondoni, Kigamboni, na Ubungo, imebaini maeneo mengi yenye fursa za uwekezaji katika sekta ya michezo na nyinginezo. Dar es Salaam imetajwa kuwa kitovu cha vivutio vya kiuchumi kinachoweza kuchochea maendeleo kuelekea mashindano makubwa ya bara la Afrika.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments