SERIKALI YATENGA BIL.114 KWA AJILI YA UKARABATI WA BARABARA ZILIZOHARIBIWA NA EL NINO KUSINI


SERIKALI YATENGA BIL.114 KWA AJILI YA UKARABATI WA BARABARA ZILIZOHARIBIWA NA EL NINO  KUSINI

#KAZIINAONGEA

Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 114 kukarabati barabara za Mikoa ya Kusini, zilizoharibiwa na mvua za El Nino, na kuitaka TANROADS kuweka taa za kutosha katika barabara kuu kuelekea Mikoa ya Kusini. 

Akizungumza katika maeneo tofauti wakati wa ziara yake Mkoani Lindi, likiwemo eneo la Somanga, 10 na 11, Januari, 2025, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuwa, kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kwa Mkoa wa Lindi ndiyo kikubwa zaidi kutengwa kuliko Mkoa mwingine wowote hapa nchini.

“ Ndugu zangu wa Lindi, nimekuja kukagua barabara zetu baada ya matatizo ya mvua za El Nino na hiki kimbunga cha Hidaya, Rais ameniagiza nije huku kuangalia hali na kuwapa pole kwa changamoto mnazopitia, kwa mapenzi yake makubwa kwenu na Watanzania kwa ujumla wake, Rais Samia ameagiza tutumie zaidi kiasi hicho cha fedha, kwa ajili ya kurekebisha barabara na madaraja yaliyoharibiwa na kutengengeza njia za kuchepusha, “ amesema Ulega.


Aidha, amesema kuwa, Mvua za El Nino zilizonyesha nchini mwishoni mwa mwaka jana zilifuatia msimu wa mvua za masika, zilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika maeneo tofauti nchini, ingawa Mikoa ya Kusini iliathirika zaidi.

Katika ziara yake hiyo, Ulega alijionea mwenyewe uharibifu uliosababishwa na mvua hizo na pia juhudi za Wakandarasi wanaojenga barabara hizo, wakiwamo Wakandarasi wazalendo.

Aidha, Waziri Ulega ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuanza kuweka taa katika barabara kuu inayoelekea Mikoa ya Kusini ili kukuza shughuli za kiuchumi katika maeneo inakopita na kwamba sera za Rais Samia ni za kukuza uchumi na kuwa maeneo ambako kuna giza ni vigumu kwa uchumi kukua.


“TANROADS naomba taa zianze kuwaka kwenye barabara hii ya kuja Kusini mwa Tanzania, haya ni maelekezo ya Rais wetu na kazi yenu ni kuhakikisha mnatekeleza agizo hilo kwa kufanya kazi usiku na mchana,” amesema.

Mbali na kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu, Ulega pia anatumia ziara hii kueleza mafanikio kadhaa yaliyopatikana kwenye eneo la ujenzi kwenye miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments