SERIKALI YAWATAKA WANANCHI KUIBUA TAARIFA ZA UKATILI
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango imetoa wito kwa Watanzania wote kuibua taarifa zinazohusu vitendo vya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Makamu wa Rais ametoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Januari 20, 2025.
Amesisitiza kuwa, wapo wanawake, watoto na wanaume wanaopitia vitendo vya ukatili wa kijinsia au kimwili lakini hawatoi taarifa kwenye vyombo vya sheria, vilevile baadhi ya mila na desturi zimekuwa zikitumika kuwakandamiza waathirika.
Pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuhakikisha usawa wa kijinsia hapa nchini, bado wanawake ambao idadi yao ni zaidi ya nusu ya watu hapa nchini, wanapewa nafasi ndogo katika umiliki wa mali na wanabaguliwa kwa msingi wa jinsia.
Ameongeza kwamba kwa mujibu wa Mpango wa Kitaifa wa Kupinga vitendo vya Kikatili dhidi ya Wanawake wa mwaka 2016, kati ya wanawake kumi, 4 wamepitia ukatili wa kimwili, na mmoja kati ya watano wamepitia ukatili wa kingono miongoni mwao wakiwa na umri mdogo (chini ya miaka 15)
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema kulingana na Ripoti ya UN Women Social Institution and Gender Index (SIGI) 2022, ukatili wa kijinsia nchini Tanzania unabainishwa zaidi kupitia ndoa za utotoni, ubaguzi ndani ya familia, ukatili dhidi ya wanawake, ukosefu wa uhuru katika kupanga uzazi, upatikanaji na umiliki wa ardhi. Pia kulingana na Taarifa ya Tathmini ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania iliyoandaliwa na Benki ya Dunia mwaka 2022, 40% ya wanawake wote wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na 17% wamepitia ukatili wa kingono.
Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejizatiti kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake hapa nchini kwa kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo inasimamia pia suala la usawa wa kijinsia. Amesema dhamira hiyo ya Serikali inaonekana zaidi kupitia mikakati, mipango na sera za kitaifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano, Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (NSGR) na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya 2000.
Ameongeza kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya kuboresha utendaji katika utoaji haki, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usawa wa kijinsia katika ngazi mbalimbali za uongozi wa Mahakama ambapo kwa takwimu, Mahakama ya Rufani, 33% ya Majaji ni wanawake, Mahakama Kuu, ni 38%. Kwa Wasajili wa Mahakama ,wanawake ni 33% na Naibu wasajili ni 48.72%. Aidha, wanawake ni 50% ya Mahakimu wa Mahakama za Mahakimu Wakazi na 41% ya Mahakimu wa Mahakama za mwanzo.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments