SERIKALI YAWEZESHA WAKUU WA SHULE, WALIMU WA TAALUMA UWEZO KUHUSU MTAALA MPYA ULIOBORESHWA


SERIKALI YAWEZESHA WAKUU WA SHULE, WALIMU WA TAALUMA UWEZO KUHUSU MTAALA MPYA ULIOBORESHWA

#KAZIINAONGEA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewezesha  utoaji elimu kwa kuwajengea uwezo kuhusu Mtaala wa Elimu ulioboreshwa, Wakuu wa shule na walimu 165 wa taaluma, kutoka shule 46 za Serikali na 19 za binafsi ili kuwawezesha walimu hao kutekeleza Mtaala huo kwa ufanisi.

Akizungumzia kuhusiana na fursa hiyo ya elimu, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mwalimu Neema Lemunge, amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia, imeiwezesha  Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, kutoa elimu kwa Walimu hao na hii ni baada ya  mtaala wa elimu kuboreshwa, ambapo Wilaya imeona kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo Wakuu wa Shule na Walimu ili waweze kuelewa na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Mbali na kuwajengea uwezo kuhusu mtaala mpya, tumefanya tathmini ya matokeo ya kidato cha pili, tumejipima, tukaona tulipo hivyo tumekubaliana na kuwekeana mikakati ya kuboresha utendaji na kuondoa matokeo duni kama daraja sifuri na daraja la nne,” amesema Mwalimu Neema Lemunge.

Afisa Elimu huyo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake za kuboresha Sekta ya elimu nchini na kwamba Serikali imejizatiti katika kujenga miundombinu ya shule ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora. 

Awali akifungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Dkt.Cainan Kiswaga amewataka walimu kutumia muda vizuri wawapo shuleni.

"Lengo letu ni kuongeza ufaulu hivyo lazima tuhakikishe kuwa tunatumia muda vizuri na tusipoteze kipindi hata kimoja" amesema Dkt.Cainan

Akifafanua kuhusu Mtaala ulioboreshwa, Mthibiti ubora wa Shule Wilaya ya Same Bw.Furahini Lubua  amesema,  kidato cha I hadi IV kutakuwa na masomo 27 ambapo haitamlazimu  mwanafunzi  kusoma masomo yote hayo kwani kutakuwa na chaguzi (option) kwa baadhi ya masomo.

Ameyataja masomo ya lazima kidato cha I hadi IV yanakuwa sita na sio Saba kama ilivyokuwa mwanzo, Masomo hayo ya lazima ni Hisabati, Kiswahili, Kiingereza, somo la biashara, Jiograpia,  Historia ya Tanzania na Maadili na kwamba somo la Bailojia na Historia yameongezwa kuwa masomo chaguzi,  yakiungana na yale ya zamani ya Fizikia na Kemia.

"Zamani Masomo chaguzi yalifanyika kwa wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne lakini kwa sasa wanafunzi wanachagua toka kidato cha kwanza, jumla mwanafunzi anatakiwa asome masomo yasiyo pungua nane na yasiyozidi kumi ambapo mtaala huo mpya utaanza Utekelezaji Januari hii 2025," amefafanua Mthibiti Ubora.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments