TARI,CIP WAWAFUNDA WAFANYABIASHARA WA VIAZI LISHE KANDA YA ZIWA



TARI,CIP WAWAFUNDA WAFANYABIASHARA WA VIAZI LISHE KANDA YA ZIWA

Kituo cha kimataifa cha viazi (CIP) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo cha Ukiriguru kimetoa mafunzo kwa wauzaji wa viazi lishe kanda ya ziwa kwa lengo la kuhamasisha biashara ya viazi lishe kwa tija na matumizi ya viazi lishe ili kuimarisha afya kwa watumiaji.

Mafunzo hayo yameshirikisha jumla ya wauzaji wa viazi lishe 12 kutoka Mikoa ya Shinyanga, Mara, Geita na Mwanza.


Akifungua mafunzo hayo yaliyobeba kauli mbiu "viazi lishe: kwa afua na kipato" Mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa kilimo TARI Ukiriguru, Dkt. Paul Saidia amesema lengo la mafunzo kujikita katika sehemu ya biashara ni kuboresha mnyororo wa thamani wa zao hilo ambalo ni muhimu sana katika kuchangia usalama wa chakula nchini hasa kipindi hiki ambacho dunia inakumbana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi.

Naye Mkurugenzi mkazi wa  Kituo cha Kimataifa cha viazi (CIP) kwa upande wa Tanzania Dkt Kwame Ogero amesema mafunzo hayo yatasaidia kuinua uzalishaji na upatikanaji wa viazi lishe hapa nchini ili kwenda kuinua pato la mfanyabiashara mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Katika mafunzo hayo washiriki wamefundishwa umuhimu wa matumizi ya viazi lishe, uvunaji na uuzaji wa viazi lishe na uhifadhi katika kuongeza thamani ya zao kwenye soko.

 Pia, kila mshiriki amepatiwa vifaa kwa ajili ya biashara hiyo ikiwemo meza, mwanvuli, visado na ndoo ili kusaidia kuendesha na kutangaza biashara ya viazi lishe katika maeneo yao.


Kwa upande wao washiriki wa mafunzo wameshukuru waandaaji wa mafunzo kwa kuwajengea ufahamu mpya kuhusu viazi lishe.

“Kwa mimi mfanyabiashara hapo mwanzo nilikuwa sifahamu nini maana ya viazi lishe, mimi na wenzangu tulikuwa tunafanya tu biashara lakini leo hii elimu hii inaenda kutuongezea ujuzi katika kulifanya zao la viazi lishe liwe la kibiashara, pia kwa kufanya hivyo tutaweza kupeleka bidhaa bora kwa mlaji.” Amesema Bw. Michael Shadrack mfanyabiashara wa viazi vitamu kutoka Mkoa wa Geita.

Post a Comment

0 Comments