#KAZIINAONGEA
Ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Jamhuri ya Watu wa Korea umechangia kuimarika kwa huduma za afya nchini katika nyanja za miundombinu ya vituo vya afya, vifaa tiba na mafunzo mbalimbali kwa watoa huduma za afya.
Hayo yameelezwa Novemba 24, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila, katika kikao kazi cha uboreshaji wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo kutoka Korea – KOFIH, kilichofanyika Jijini Dodoma.
Rumatila amesema, katika kipindi cha miaka mitano (5), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imenufaika na ushirikiano uliopo kati yake na Korea kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (HSSP-IV) pamoja na Mpango Mkakati wa Tano (5).
“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Korea na Taasisi yenu, Shirika la Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH), kutokana na msaada wenu endelevu kwa Serikali ya Tanzania, hususan kwenye Sekta ya Afya, tukio la leo ni ushuhuda wa juhudi za kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi zetu mbili,” amesema Bw. Rumatila
Ameongeza kuwa Tanzania na Korea zimeazimia kuendelea kuboresha Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma kwa ajili ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, kuimarisha usimamizi wa hospitali, pamoja na ukarabati na ujenzi wa wodi maalum za watoto wachanga wagonjwa (NICU).
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la KOFIH Tanzania, Bw. Gyeongbae Seo, amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments