VIONGOZI KUTOKA HALMSHAURI YA WILAYA YA CHATO WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO SHAMBA LA MITI SAOHILL
Na Mwandishi wetu, Iringa
Leo tarehe 13 Januari 2025 viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Peter Bura, Katibu Tawala wa Wilaya pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo wamefanya ziara ya mafunzo katika Shamba la Miti Saohill lililopo katika Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa.
Akizungumsha wakati wa ukaribisho wa Viongozi hao Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt Linda Salekwa amewapongeza kwa kuchagua kuja kutembelea na kujifunza kuhusu uhifadhi wa misitu utunzaji mazingira na ukusanyaji wa mapato katika Wilaya ya Mufindi kwani ni eneo sahihi kwao.
"Tunapozungumza habari ya uhifadhi wa mazingira, na ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na serikali, Wilaya ya Mufindi imepiga hatua kubwa sana na hii inatokana na uwepo wa Shamba la miti la serikali la Saohill" amesema
Ameongeza kuwa kupitia elimu inayotolewa na wahifadhi kuhusu utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti imechangia uwepo wa rasilimali kubwa ya misitu hali iliyopelekea kuwepo kwa viwanda vingi vinavyochakata mazao ya misitu hivyo kuongeza pato la serikali kutokana na ushuru unakusanywa kupitia halmashauri.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Peter Bura amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza ni kwa namna gani Wilaya ya Mufindi kupitia Shamba la Miti Saohill wamefanikiwa katika uhifadhi wa mazingira na ukusanyaji wa mapato ili nao waweze kuona ni hatua gani watazichukua katika kufanikisha hilo katika Wilaya ya Chato.
"Katika Wilaya ya Chato tunalo Shamba la Miti Silayo hivyo tumekuja kujifunza ni kwa namna gani wenzetu wa Mufindi wananufaika vipi kimazingira na kimapato ili na sisi tuone ni kwa namna gani kupitia Shamba la Miti Silayo tutashirikiana na TFS katika kuleta tija katika wilaya yetu kupitia Shamba lile" amesema
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Saohill PCO Tebby Yoramu amesema kuwa Shamba limefanikiwa kufika hatua iliyopo kwa sasa kutokana na kuwepo kwa programu mbalimbali zinazolenga kutengeneza mahusiano mazuri na jamii zinazolizunguka shamba iliwemo kutoa ajira kwa wanachi, elimu ya uhifadhi pamoja na kusaidia shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu na miondombinu ya barabara hali inayopelekea kuwepo kwa uhusiano chanya baina ya shamba na wananchi.
Katika ziara hiyo Viongozi kutoka halmashauri ya Wilaya ya Chato waliweza kujifunza juu ya shughuli mbalimbali za ufugaji nyuki, uzalishaji wa miche katika bustani, pamoja na shughuli za uvunaji wa utomvu katika misitu.
Mwisho
0 Comments