Wafanyabiashara wa mbolea nchini wametakiwa kuzingatia bei elekezi iliyowekwa na Serikali


Wafanyabiashara wa mbolea nchini wametakiwa kuzingatia bei elekezi iliyowekwa na Serikali

Wafanyabiashara wa mbolea nchini wametakiwa kuzingatia bei elekezi iliyowekwa na Serikali na kuzingatia uuzaji wa mbolea kupitia mfumo wa ruzuku, sambamba na kutii sheria ya mbolea bila shuruti.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Joel Laurent wakati wa kufunga mafunzo kwa maafisa udhibiti ubora.

Laurent amesema kuwa ipo tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara wa mbolea wasio na uaminifu wanaouza mbolea tofauti na bei elekezi jambo ambalo ni kosa kisheria. 


Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo amewaonya wanaohujumu tasnia ya mbolea kwa namna yotote ile na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa atakayebainika ikiwemo kuwatoza faini au kufungia leseni za biashara zao.

Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Afisa udhibiti ubora mkuu Gerold Nganilevanu amewataka wakaguzi wa mbolea nchini kutilia mkazo utekelezaji wa utozaji wa tozo ya adhabu ya papo kwa papo kwasababu ni eneo muhimu wanalofanyia kazi mara kwa mara ikilinganishwa na maeneo mengine.


Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo kaimu meneja wa huduma za sheria TFRA Fikiri Mboya amewataka wakaguzi wa mbolea kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya mbolea namba 9 ya mwaka 2009.

Mboya amesema kuwa miongoni mwa majukumu ya wakaguzi wa mbolea ni kuhakikisha shughuli za udhibiti zinatekelezwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria.


Aidha Mboya amebainisha kuwa kwa mujibu wa sheria, mamlaka imepewa nguvu kisheria kushughulikia makosa bila kwenda mahakamani kwa makosa yasiyo na madhara makubwa

Mafunzo hayo ya ndani yamefanyika leo makao makuu ya TFRA jijini Dar es salaam kwa njia ya mtandao kwa maafisa udhibiti ubora wa kanda zote za Mamlaka, kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao na kuhakikisha sheria ya Mbolea inatekelezwa bila shuruti na Mbolea bora inaendelea kuwafikia wakulima.

Post a Comment

0 Comments