WAKULIMA WAUNGA MKONO JUHUDI ZA TFS RAIS SAMIA WAPANDA MITI 1,000
Mwandishi wetu, Mbeya
Wakulima zaidi ya 500 wa kitongoji cha selemba mtaa Itezi Mlimani Kata ya Nsalaga Jijini Mbeya wamepanda miti 1,000 kwenye vyanzo vya maji katika safu ya Mlima Kawetire kama kuunga mkono kinara wa utunzaji Mazingira Rais Samia Suluhu Hassan .
Zoezi hilo limetajwa kwenda sambamba na kumpongeza Rais wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuelekea siku yake ya kuzaliwa Ijumaa Januari 27 mwaka.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima Sarah Japhet,amesema hatua ya kupanda miti 1,000 ni ishara ya kuishukuru serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu(TFS) kuwarejeshea sehemu ya eneo la mlima Kawetire lilikuwa na mgogoro kwa zaidi ya miaka nane.
"Tutaendelea kushirikiana na TFS kutunza maeneo tuliyo rejeshewa kwa kupanda miti rafiki kwenye vyanzo vya maji ili kutunza mazingira , kupata maji na kuongeza tija ya kilimo cha umwagiliaji katika safu ya mlima huo ambalo ni tegemeo kwa chakula,"amesema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Itezi mlimani ,Tegemeo Moto,amesema wanaishukuru serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu( TFS) kwa kutoa miti kwa ajili ya kupanda kwenye vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
"Tunaona mabadiliko ya tabia nchi yanavyo athiri shughuli za kilimo kufuatia shughuli za kibinadamu na ukataji miti ovyo ,kupitia zoezi hilo la upandaji miti tunakwenda kuwa wasimamizi ili kurejesha mvua na uoto wa hasili kwenye vyanzo vya maji,"amesema
Kaimu mtendaji wa mtaa wa Itezi Mlimani Ezra Chaula ,amesema wanaishukuru serikali kwa kuridhia sehemu ya eneo hilo kurejeshwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na kuwataka kutofanya uharibifu wa kulima ndani ya mita 60 ya vyanzo vya maji.
" Tunamshukuru Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge kukutana na pande zote mbili hatimaye TFS kurejesha wananchi sehemu ya eneo kwa ajili ya kuendeleza kilimo,"amesema
Chaula ameomba TFS kuendelea kutoa miti kwa wakulima ili kuendeleza kampeni ya upandaji miti kwenye vyanzo vya maji kwa lengo la kutunza mazingira na kudhibiti athari ya mmonyoko wa udongo.
Katibu wa kikundi cha Wakulima hao,Crispin Kandi amesema kitendo cha TFS kuridhia kurejesha eneo la kilimo kwa wameonyesha uzalendo wa kuwajali wananchi ambao utegemea safu mlima huo kuzalisha mazao ya kilimo na biashara.
Mhifadhi Mkuu wa shamba la miti Kawetire linalo simamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) , Arnold Shoo amesema katika kuhakikisha wananchi wanatunza mazingira wataendelea kutoa miti ya aina mbalimbali.
"Tumetoa miti zaidi ya 1,000 kwa wakulima wa eneo hilo lengo ni kuona wanatunza mazingira katika safu ya Mlima Kawetire kwa ajili ya kutunza uhifadhi wa miti na vyanzo vya maji ili kudhibiti mmonyoko wa udongo unaotokana na shughuli za kilimo "amesema Shoo.
Awali , Shoo amesema anashukuru serikali kupitia uongozi wa juu wa TFS na Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini,Dkt ,Tulia Ackson kuridhia sehemu ya eneo kurejesha kwa wananchi kwa ajili ya kilimo .
Wakati huo huo ,Shoo amewataka wananchi wanaolima kwenye maeneo ya hifadhi za misitu kuacha tabia na uchomaji ovyo moto pindi wanapoandaa mashamba na badala yake watumie askari wa TFS ili kudhibiti majanga ya moto yanayojirudia mara kwa mara na kusababisha hasara.
Mwisho.
0 Comments