WANANCHI MBAMBA BAY WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUWAJENGEA BARABARA ZA MITAA


WANANCHI MBAMBA BAY WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUWAJENGEA BARABARA ZA MITAA

#KAZIINAONGEA

Wakazi wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wakala wa Barabara za vijijini na mijini(TARURA) kwa kuboresha miundombinu na kujenga Barabara za Mitaa katika Mji mdogo wa Mbamba bay kwa kiwango cha lami.

Wakisifu jitihada za Rais Samia katika utawala wake ndani ya miaka mitatu tangu alipoingia madarakani, wamesema kuwa hapo awali, wakazi wa Mbambabay walikuwa wakikutana na adha ya usafiri na kwamba,   tangu barabara hizo zilipojengwa, imesaidia kurahisisha huduma ya usafiri kutoka sehemu moja  kwenda nyingine na kuondoa adha ya vumbi kipindi cha kiangazi na matope kila inapofika msimu wa mvua pamoja na maeneo yao kupanda thamani.

Petro Zambala mkazi wa Mbambabay amesema, uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika Mji huo, utaharakisha maendeleo  na kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Wilaya ya Nyasa ambapo kabla ya barabara za lami baadhi ya huduma za kijamii zilipatikana kwa shida, kutokana na kushindwa kufika maeneo ya kutolea huduma hizo kwa wakati, jambo lililosababisha kuwa na maisha magumu.

Mkazi mwingine wa Mbambabay Nikaya Mbalale amesema,tangu Serikali ya Rais Samia ilipoingia madarakani, kuna mabadiliko makubwa katika Mji huo, hasa baada ya TARURA kupatiwa fedha nyingi ambazo zimewezesha kuboresha miundombinu ya barabara zake kwa lami, tofauti na siku za nyuma ambapo barabara nyingi za mitaa zilikuwa za vumbi na kwamba, barabara hizo zimehamasisha na kuwavutia watu wengi kwenda kuwekeza katika Mji wa Mbambabay  ambao wananchi wake wanategemea shughuli za uvuvi na kilimo ili kuendesha maisha yao.

Aidha Mbalale, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha kukamilisha ujenzi wa mradi wa barabara ya Mbambabay-Mbinga yenye urefu wa kilometa 66 kwa kiwango cha lami ambapo kukamilika kwa barabara hiyo, kumesaidia kupunguza gharama za maisha na usafiri kwani  hapo awali  walikuwa wanalipa nauli Shilingi 15,000 kutoka Mbambabay hadi Mbinga lakini kwa sasa wanalipa Shilingi 9,000 hadi 10,000.

Amesema, tangu TARURA ilipoboresha miundombinu kwa kujenga barabara za lami na mifereji ya kupitisha maji wananchi wanaishi kwa amani na wanapata muda wa kufanya shughuli za kuwaingizia kipato bila hofu badala ya kubaki nyumbani pindi mvua zinaponyesha ili kuokoa mali zao zisisombwe na maji.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Nyasa, Derick Theonest amesema kuwa, TARURA inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kwa kujenga barabara za lami ili kuboresha mazingira na maisha ya wananchi wa mji wa utalii wa Mbambabay na wilaya ya Nyasa kwa ujumla.

Amesema, hadi sasa wamebakisha kilometa moja ili kukamilisha barabara za lami katika Mji wote wa Mbambabay na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuipatia TARURA fedha kwa kujenga miundombinu ikiwemo barabara za lami ambazo zina mchango mkubwa katika kuchochea na kuharakisha maendeleo na kuwataka wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya barabara hizo ili zidumu kwa muda mrefu kwani zinatumia fedha nyingi kuzitengeneza.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments