WATANZANIA WATAKIWA KUTOHOFIA KUTUMIA NISHATI YA UMEME KUPIKIA
#KAZIINAONGEA
Watanzania kote nchini, wametakiwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya Nishati ya kuni na mkaa, badala yake wanatakiwa kutumia Nishati ya gesi na umeme katika kupikia, kwa lengo la kulinda afya na mazingira.
Wito huo umetolewa na Afisa Mwandamizi wa Shirika la Umeme nchini, (TANESCO), Carol Makundi, Jumamosi,Januari 11, 2025 katika hafla maalumu ya Uhamasishaji na Kutoa Elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Viongozi wa Dini ya Kiislam Jijini Arusha, inayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), chini ya uratibu wa Mbunge wa Arusha Mjini. Mrisho Gambo.
Makundi amesema kuwa, matumizi ya umeme katika kupikia yanaweza kusaidia kupunguza gharama za maisha, kulinda mazingira, na kuboresha afya za Wananchi na kwamba Watanzania wengi wamekuwa wakihofia kutumia umeme kama nishati ya kupikia kwa kudhani kuwa gharama zake ni kubwa, na kwamba Shirika la Umeme limeeleza kuwa, umeme si tu nishati rahisi na salama bali pia ni suluhisho endelevu kwa changamoto za kupikia nchini.
Makundi ametoa mfano wa gharama zinazotumika kupika katika Nishati tofauti kuwa, nusu kilo ya maharage , kwa matumizi ya umeme yanaweza kushusha gharama hiyo hadi Shilingi 200 pekee, ikilinganishwa na Shilingi 1,200 kwa mkaa, Shilingi 800 kwa LPG, na Shilingi 600 kwa mafuta ya taa na kwamba, kupikia kwa umeme si tu nafuu bali pia kuna mchango mkubwa katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa kaboni na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Katika hafla hiyo, TANESCO imeeleza mikakati yake ya kukuza matumizi ya nishati safi nchini, ikiwemo kutoa elimu kwa watumiaji wa kawaida, viongozi wa dini, na wadau wengine kuhusu faida za kupika kwa umeme, ambapo Shirika hilo limekuwa likifanya tafiti kubaini vifaa bora vya kupikia vinavyotumia umeme kidogo ili kupunguza gharama za awali kwa watumiaji, huku likishirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wizara ya Nishati katika kusukuma mbele ajenda ya Nishati safi inayotoliwa mkazo na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
*#KAZIINAONGEA*
0 Comments