Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Balozi. Habibu Awesi Mohamed amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Bodi ya Chai Tanzania (TBT) katika kuiendeleza sekta ya chai huku akiahidi kushirikiana na bodi hiyo katika kuinadi chai ya Tanzania nchini Qatar.
Balozi ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya uongozi wa TBT ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wake, Bi. Beatrice Banzi kuhudhuria Maonesho makubwa ya bidhaa za kilimo, mifugo na huduma nyinginezo yaliyofanyika nchini Qatar.
Amesema kuwa ni wazi kuwa ushiriki wa TBT katika maonesho hayo unafungua milango ya mauzo ya chai ya Tanzania kwenda kimataifa zaidi hasa ikizingatiwa kuwa chai ya Tanzania inasifa za kipekee.
Anasema,”Ujio wa Bodi ya Chai hapa nchini qatar umeonesha ni kwa namna gani Tanzania ilivyojipanga kuliteka soko la chai la Qatar hasa kwa kuzingatia kuwa wazawa wa hapa Qatar wanakunywa chai zaidi kuliko kinywaji kingine chochote".
Anaongeza,"nimeshuhudia namna ambavyo Bodi ya chai Tanzania imezitangaza aina mbalimbali za chai kutoka kampuni mbalimbali za uchakataji wa chai Tanzania, wakiwa kwenye maonesho haya wawekezaji kwenye kampuni kadhaa za chai hapa Qatar walipata wasaha wa kuionja chai za Tanzania".
Mheshimiwa Balozi anasema kuwa Chai ya Tanzania imekubaliwa kuuzwa katika maduka makubwa ya bidhaa ya nchini Qatar yani katika Supermarkets za Jiji la Doha kama vile Saudi Hypermarket, Lulu Hypermarket, Family Food Supermarket pamoja na wafanyabiashara wengine wakubwa wa hapa nchini Qatar.
“Naisihi Bodi ya Chai kuendelea kuwekeza kwenye tasnia hii ya chai hasa kwa kuimarisha yale yote yanayotakiwa kwa kuwa sekta ya chai hasa chai ya Tanzania inasoko kubwa hapa Qatar” amesema Balozi.
Anabainisha zaidi kuwa mbali na chai pia kulikuwa na mazao mengine kutoka Tanzania na pia Maafisa kutoka Bodi, Wizara na Halmashauri mbalimbali za Tanzania walishiriki.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TBT, Bi. Beatrice Banzi amebainisha kuwa kupitia sera inayotekelezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya diplomasia ya Uchumi imefungua milango zaidi ya kuinadi chai ya Tanzania katika mataifa mbalimbal na matokeo yanaendelea kuonekana hususan katika sekta ya chai.
0 Comments