MIRADI YA RAIS SAMIA YAZIDI KUSHAMIRI


MIRADI YA RAIS SAMIA YAZIDI KUSHAMIRI

Jengo la Hazina -  Geita lazinduliwa

Seikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mbali na kuanzisha miradi mipya, pia Serikali ya Rais Samia imekamilisha miradi  iliyoachwa na mtangulizi wake.

Miongoni mwa miradi inayoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita ni ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi Mwanza.

Ndani ya mkoa wa Geita Serikali ya Rais Samia imetekeleza miradi kadhaa ukiwemo wa Mabweni ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, Zahanati, nyumba za watumishi, upanuzi wa kituo cha Afya Bulela sambamba na mradi wa jengo la Hazina ambao umekamilika.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Haroon Nyongo amezindua rasmi Jengo hilo la Hazina Mkoa wa Geita kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba  na kusisitiza umuhimu wa  Watanzania kuwa na nidhamu ya fedha, kukopa kwa ajili ya mahitaji yenye tija na kuchukua mikopo  kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali ili kuepukana na janga la mikopo umiza.


Uwepo wa Ofisi za Hazina Ndogo mkoa wa Geita  itawapunguzia Wananchi adha ya kutembea umbali mrefu na gharama ili kupata huduma pamoja na kuwasaidia kupata elimu ya kifedha kutoka kwa watumishi wa Hazina.

Aidha, Nyongo, imeiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ofisi zote zinazoshughulika na usimamizi wa sekta ya fedha na Kamati  zote za Ulinzi na Usalama kufuatilia kwa ukaribu taasisi zote zinazotoa mikopo nchini.

Amesema kuwa changamoto ya mikopo umiza imekuwa ni ya muda mrefu na inaendelea kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wa kawaida na kwamba ni lazima hatua zichukuliwe haraka kukomesha tatizo hilo.

"Naelekeza kuchukua hatua kali dhidi ya wanaotoa huduma za fedha bila leseni na kuwanyanganya leseni wote watakaobainika wanatoa mikopo bila kuzingatia mashariti ya leseni.

Pia, ametoa onyo kwa watu binafsi na kampuni zinazojihusisha na utoaji wa mikopo ya namna hiyo kuacha mara moja kwani jambo hilo linarudisha nyuma Wananchi.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, amesema Jengo hilo lina Ofisi 14 zitakazotumika na watumishi 50 na litatumiwa na Idara mbili ambazo ni Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali na Hazina Ndogo Mkoa wa Geita pamoja na Ofisi ya Takwimu Mkoa wa Geita.

“Jengo hili litaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wetu, na wateja wetu, itapunguza gharama za uendeshaji wa Ofisi hususani kukodi kwa maana ya kulipa pango", amesema Mwenda.

Mshauri Elekezi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),  Bi. Amina Lumuli, amesema kuwa mradi wa Jengo la Hazina Ndogo Geita umetekelezwa na Mkandarasi Masasi Construction Co. Ltd. pamoja na TBA ambaye ni Mshauri Elekezi.


“Mradi ulianza Juni 30, 2023 na kukabidhiwa Desemba 03, 2024 ambapo mradi huu ulikuwa wa miezi 15, gharama za mradi ni sh  bilioni 4.37 pamoja na VAT gharama za Mshauri Elekezi ni sh milioni 269", amesema Bi. Lumuli.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bw. Hashimu Komba amesema kuwa uwepo wa Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Geita itaondoa usumbufu kwa wananchi kufuata huduma za Hazina mkoani Mwanza.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments