SERIKALI YAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WATUMISHI, WANAVIKUNDI NA WAJASIRIAMALI


SERIKALI YAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WATUMISHI, WANAVIKUNDI NA WAJASIRIAMALI 

#KAZIINAONGEA

Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha imewajengea uelewa wa Elimu ya Fedha Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Wanavikundi na Wajasiriamali wadogo wadogo walioshiriki katika semina zinazoendelea katika Kata, Wilaya mbalimbali Mkoani Kilimanjaro.

Semina hiyo ya Elimu ya Fedha iliyotolewa kwa Watumishi ilifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, na kwa Wanavikundi na Wajasiriamali wadogo wadogo ilifanyika katika Ukumbi wa Family Conference Hall na Ofisi ya Tarafa ya Siha Kati, Kata ya Fuka Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro.

Akiikaribisha Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Bw. Haji Mnasi, amesema kuwa amefurahishwa na ujio wa Timu hiyo kuja kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya Uwekaji Akiba, Mikopo na Uwekezaji kwani ni fursa kubwa kwa watumishi wa Halmashauri yake.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Elimu ya Fedha kwa Watumishi wa Halmashauri ya Siha Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, amesema ni vyema watumishi wa umma wakatumia elimu hiyo ya fedha ili kuboresha matumizi yao ya kila siku na kuweka akiba ili kuepuka kuchukua mikopo kausha damu.

“Elimu hii itawawezesha kufahamu ni wakati gani unatakiwa kuchukua mkopo na namna bora ya kuutumia, pia itawawezesha kufahamu mahali salama kwa kuwekeza fedha kidogo kidogo ili kuboresha hali ya uchumi na kuwaondolea mawazo ya kukopa kila wakati.” Amesema Bw. Kimaro.

Aidha, Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga,  amewahimizi Watumishi wa Umma, Wanavikundi na Wajasiriamali wadogo wadogo kujijengea utamaduni wa kuweka akiba kila wanapopata kipato ili iwasaidie kuwaongezea katika uwekezaji na kukuza uchumi.

Bw. Mwanga amesema kuwa ili kuweka akiba ya fedha ni vyema wakabainisha matumizi yasiyo ya lazima na kuyaondoa na kufanya akiba kuwa ni sehemu ya matumizi ya lazima kila wanapopata fedha.

“Ukiwa na utamaduni wa kuweka akiba, suala la kuwekeza fedha linakuwa ni rahisi, na unaweza ukawekeza kwenye kilimo, biashara, na Masoko ya Mitaji ikiwemo Hisa na Hati Fungani ili kuiwezesha akiba yako unayoitunza kukua na kuongezeka” Amefafanua Bw. Mwanga.


Katika kuhitimisha semina ya Elimu ya Fedha kwa Watumishi, Wajasiriamali na Wanavikundi, Afisa Usimamizi Fedha Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bw. Jackson Mshumba, amesema kuwa Serikali inajua kuwa kuna changamoto kubwa zinazotokana na uelewa mdogo wa elimu ya fedha hasa katika masuala ya mikopo kuwa na riba kubwa na kusababisha migogoro kwenye familia mara mikopo hiyo inaposhindwa kulipika.

“Tunawaomba watumishi na wananchi kwa ujumla watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa mara tu wanapobaini kuwa kuna watoa huduma za fedha ambao wanakiuka utaratibu wa kisheria ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria” Amesema Bw. Mshumba.

Semina ya Elimu ya Fedha Imetolewa Wilayani Siha,  Mkoani Kilimanjaro kwa Machinga, Wakulima, BodaBoda, Mama/ Baba Lishe na Vikundi vya Huduma ndogo za Fedha.

*#KAZIINAONGEA*

Post a Comment

0 Comments