SERIKALI YAITAKA MSD KUSIMAMIA UENDESHAJI WA VIWANDA VYA NDANI VYA BIDHAA ZA AFYA
#KAZIINAONGEA
Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Afya imeitaka Bohari ya Dawa nchini (MSD) kusimamia viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa za afya ikiwemo dawa, maji dawa (drip) ili kuviwezesha viwanda hivyo kuendelea kukua na kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hayo yamejiri hivi karibuni wakati Waziri wa Afya Jenista Mhagama alipotembelea viwanda vinavyozalisha bidhaa za afya ikiwemo kiwanda cha Pharmaceutical, Medical Devices, Medical Equipment Assembly, Raw materials (API), Common Utilities pamoja na Logistic Centre (Warehousing) vilivyopo Zegereni, kibaha mkoani Pwani.
Waziri Mhagama amesema, pamoja na kujenga historia ya Taifa hili, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezielekeza sekta binafsi kuhakikisha zinachangia katika ujenzi wa uchumi, ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania.
"Hata sisi leo, tumekuja kuona wenzetu wa Sekta binafsi ni namna gani wanaweza kutumika kwenye maendeleo na hasa upande wa sekta ya afya, lakini tunajua kuna uwekezaji mkubwa mkoa wa Pwani ambao una zaidi ya viwanda 100 vilivyojengwa ndani ya muda mfupi," amesema Waziri Mhagama.
Amesema, Sekta ya Afya inauhitaji mkubwa wa uwekezaji wa viwanda nchini kwa kuwa kwenye bara la Afrika zaidi ya asilimia 70-80 bidhaa za afya zinatoka nje ya nchi ingawa kuna changamoto ya ucheleweshaji wa bidhaa za afya kutoka nje, hivyo kuna manufaa bidhaa za afya zinapozalishwa nchini, ikiwemo kupunguza gharama kubwa ya bajeti ya nchi.
Amesema, faida nyingine za uzalishaji wa bidhaa hizo nchini ni pamoja na kupunguza utegemezi, kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa hizo kwa kuzingatia mahitaji na matumizi ya nchi, kuchagua ni bidhaa gani ambazo zinahitajika zaidi pamoja na kuhifadhi fedha za kigeni ili zitumike kwenye uwekezaji wa maeneo mengine.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali inaanza kujipanga kuanza mkakati wa kuuza bidhaa za afya nje ya nchi kwa kuwa tayari Serikali ya Tanzania imepata masoko ya kuuza bidhaa hizo nje ya nchi.
"MSD imepata mamlaka ya kusambaza bidhaa za afya kwenye soko la SADC, ni lazima sasa MSD ikae na wazalishaji wa ndani, badala ya bidhaa hizo kuziagiza nje ya nchi," amesema Waziri Mhagama.
#KAZIINAONGEA
0 Comments