TAASISI ZA KILIMO ZATAKIWA KUBADILI MTAZAMO NA KUHAMASISHA KILIMO BIASHARA ILI KUONGEZA TIJA



TAASISI ZA KILIMO ZATAKIWA KUBADILI MTAZAMO NA KUHAMASISHA KILIMO BIASHARA ILI KUONGEZA TIJA

Taasisi za kilimo nchini  zimetakiwa kubadili mtazamo nakuja na mbinu mpya ya  kuwawezesha wakulima kuongeza tija katika kuendesha kilimo cha biashara.

Akizungumza katika ziara ya Bodi na Menejimenti ya TFRA Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo alipotembelea taasisi mbalimbali za Wizara ya Kilimo, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI – Maruku), Kituo cha Uhaulishaji Teknolojia za Kilimo (MATI – Maruku), na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI). 

Amesema kuwa Ziara hiyo inalenga kuelewa majukumu ya taasisi hizo na kuimarisha ushirikiano katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea miongoni mwa wakulima.

Dkt. Diallo amesisitiza kuwa ili kufanikisha malengo ya serikali kupitia kauli mbiu ya Agenda 10/30: Kilimo ni Biashara, wataalamu wa kilimo wanapaswa kuongeza jitihada katika kutoa elimu na ushauri kwa wakulima ili kubadili mitazamo hasi kuhusu matumizi ya mbolea na kuchochea uzalishaji wenye tija kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, ameeleza kuwa, ziara hiyo imetoa fursa kwa TFRA kufahamu kwa undani zaidi shughuli za taasisi hizo na kutathmini maeneo ya ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea. 

Amebainisha kuwa TFRA inajumuisha wakufunzi wa MATI katika programu zake za mafunzo kwa wakulima, ili kuwawezesha wakufunzi hao kuendeleza utoaji wa elimu kwa wakulima kwa ufanisi pindi mafunzo yanapohitajika.

Katika wasilisho lake, Meneja wa TARI – Maruku, Dkt. Mpoki Shimwela, ameeleza kuwa, matumizi duni ya mbolea katika kilimo cha migomba yamesababisha upungufu wa virutubisho kwenye udongo, hali inayochangia kuzalisha ndizi kilo chache na zisizo na ubora unaokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa

Post a Comment

0 Comments